WAKATI msafara wa watu 30 wakiwemo wachezaji
na viongozi wa timu ya soka ya Al Ahly Shandy ya Sudan ukiwasili nchini leo kwa
ajili ya kukwaana na Simba, mgeni rasmi katika mechi hiyo anatarajiwa kuwa
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Timu hizo zitakwaana Aprili
29 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa 16
bora ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).
Akizungumza mara baada ya
kuwasili kwenye uwanja wa Kimataifa wa Mwl. JK Nyerere, kocha mkuu wa Al Ahly
Kouk Mohammed aliiambia mamapipiro blog kwamba mchezo huo uantarajiwa kuwa na ushindani mkubwa
kwani Simba ni timu nzuri.
Alisema anaifahamu Simba
kama moja ya timu mahiri barani Afrika sambamba na kuwa na uzoefu wa kucheza
michuano ya kimataifa hali ambayo itawafanya wawe makini zaidi pindi
watakaposhuka dimbani.
Hata hivyo kocha huyo raia
wa Tunisia alisema kwamba huenda wakaathiri kidogo na hali ya hewa ya Tanzania
kutokana na kuwa tofauti na Sudan ingawa watajitahidi kukabiliana
nayo.
Kikosi cha Al Ahly kinaundwa na wachezaji
watano wa kimataifa wakiwemo wawili kutoka Nigeria , mmoja kutoka Mali na
mwingine kutoka Mali huku wachezaji wawili wakiichezea timu ya Taifa ya Sudan
.
Al Ahly wanakutana na Simba
baada ya kuitoa Ferroviario ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-0, huku Simba
iliitoa Es Setif ya Algeria huku Simba ikibebwa na bao la ugenini baada ya
nyumbani kushinda 2-0 kabla ya kwenda kufungwa 3-1.
Katika hatua nyingine
tiketi kwa ajili ya kushuhudia mpambano huo zinatarajiwa kuanza kuuzwa leo
katika vituo tofauti jijini Dar es salaam huku waamuzi wa mchezo huo kutoka
Swaziland Nhleko Simanga Pritchard, Mbingo Petros Mzikayifani,Sibandze Thulani,
Fakudze Mbongiseni Elliot na Kamishna wa Kayijuga Gaspard wa
Rwanda wanatarajiwa kuwasili leo.
Katika kujiandaa na mchezo
huo, Simba imepiga kambi eneo la Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam ambapo
kocha mkuu wa Simba Mserbia Milovan Cirkovic amejinasibu kushinda mchezo huo ili
kujiweka katika mazingira mazuri kwenye mchezo wa marudiano
utakaopigwa wiki mbili zijazo katika jiji la Shandy , Sudan .