LICHA ya kuwa muziki wa bongo fleva/Hip hop bado umekuwa hautiliwi maanani hapa nchini kama unaweza kusaidia kuleta mabadiliko katika jamii, baadhi ya wasomi wameanza kuifuta dhana hiyo.
Wameanza kuchukua hatua hiyo kwa kuhakikisha wanausomea muziki huo, na kutunikiwa shahada za juu katika vyuo vikuu hapa nchini ama nje ya nchini.
Mmoja ya watu walioamua kuchukua hatua hiyo muhimu kwa maendeleo ya muziki huo, ni mwanadada Dkt. Shani Omari ambaye ametunukiwa shahada ya udaktari wa muziki wa hip-hop (PHD) mwaka 2009, katika chuo kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mwanamke na muhitimu wa kwanza hapa nchini kutunukiwa shahada hiyo.
Dk. Shani alipata mwamko wa kusomea Shahada hiyo, baada ya kuona muziki huo unadharauriwa hapa nchini licha ya kujulikana sana duniani.
Anasema uamuzi wa kuusomea zaidi muziki huo ulitokana na kuwa na mapenzi nao tangu akiwa mwanafunzi, hasa alipokuwa akisoma sekondari huku akipenda zaidi muziki wa kufokafoka ‘rap’ kuliko mitindo mingine, hususan michanio ya lugha ya Kifaransa.
“Nilimaliza kidato cha sita katika sekondari ya Zanaki mwaka 1994 na mwaka 1995 nilijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam, nikasomea Shahada ya kwanza ya sanaa katika Elimu (BA Education) na kuhitimu mwaka 1999. Mwaka 1999 hadi 2002, nilisomea shahada ya Uzamili katika Isimu chuoni hapo,” Anasema.
Aidha, mwaka 2005- 2008 alikuwa katika Chuo Kikuu cha California nchini Marekani akifanya utafiti wa bongo Fleva, kabla ya kurejea nchini mwaka 2009 na kutunukiwa shahada yake ya Udaktari (Phd ya hip-hop).
Kutokana na kuwa na lengo ya kuendeleza muziki hapa nchini, siku kadhaa baada ya kutunukiwa shahada ya udaktari wa hip-hop, Dkt. Shani kwa kushirikiana Taasisi ya Taaluma za Kiswahili kupitia Kituo cha Fasihi ya Kiswahili, Mapokeo Simulizi na Andishi ya Kiafrika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliandaa Tamasha la ‘Elimika na Bongo Fleva’.
Tamasha hilo ambalo lilifanyika Januari 16 na 17 mwaka huu wa 2010 katika ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, liliwakutanisha wanataaluma, wasanii, waandaaji, wasambazaji, mapromota, wachezesha muziki ‘ma-dj’, wanahabari, wanafunzi na jamii kwa ujumla, ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu muziki wa vijana Tanzania.
Tamasha hilo lilikuwa na madhumuni ya kuutambua kitaaluma mchango wa wasanii wa Bongo Fleva na wadau wake katika maendeleo ya vijana, sanaa, Kiswahili, utamaduni na jamii kwa ujumla.
Kupitia tamasha hilo wasanii walipata fursa ya kuonyesha kazi za sanaa, kuwasilisha makala kulikofanywa na wasanii, wanataaluma na wadau mbalimbali, pia mashindano ya wasanii wachanga, majadiliano na burudani.
Likibeba kauli mbiu ya ‘Bongo fleva kwa maendeleo yetu’ tamasha hilo lilitoa nafasi kwa vijana katika kuleta maendeleo na kukuza utamaduni nchini.
Lengo la tamasha kuupa hadhi muziki huo lilitimia kwa kuwa tofauti na wengi wanavyodhania, ukweli ni kuwa mtindo huo umeanza tangu vizazi vya kale kupitia ngonjera ambayo kimsingi ni kufokafoka kwa midundo ya ngoma za asili.
Baadhi ya wasani wa muziki wa bongo fleva walioshiriki wakiwemo Joseph Mbilinyi ‘Mr II’ a.k.a Sugu, Seleman Msindi ‘Afande Sele’, G.Solo, Fred Malik ‘Mkoloni’, Zay-B, Slaughter na wengineo
Dk. Shani alizaliwa jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa miaka ya 1970 na kupata elimu ya msingi katika shule ya Kurasini mwa 1981- 1987, 1988-1991 akasoma sekondari ya Kibasila na 1992-1994 alisoma kidato cha tano na sita katika sekondari ya Zanaki.
Anawashauri wasanii kutambua kuwa wana nafasi kubwa ya kuielemisha na kuifunza jamii kupitia muziki, si katika kuimba tu bali pia kushirikiana na wadau mbalimbali na si mapromota na watayarishaji wa muziki tu.