Na Brown Jonas – WUSM, Ivory Coast
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro ametembelea Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Laurent Pokou uliopo jijini San Pedro nchini Ivory Coast ili kujifunza na kuona namna ambavyo nchi hiyo imefanya maandalizi ya uenyeji wa AFCON 2023 ikiwemo ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mashindano hayo makubwa Afrika.
Dkt.Ndumbaro amefanya ziara hiyo sanjari na kuhudhuria mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon2023) yanayoendelea nchini humo kama sehemu ya Tanzania kuendelea kujiandaa na uenyeji wa mashindano hayo mwaka 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Dkt. Ndumbaro amesema aina ya uwanja aliouona unafaa pia katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ambapo amesema Serikali mbali na kuendelea kujenga viwanja vya michezo Dodoma na Arusha inaendelea kukaribisha wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo katika ujenzi wa miundombinu ya michezo katika mikoa mingine.
Katika ziara hiyo,Dkt. Ndumbaro ameambatana na Kaimu Balozi wa Kituo cha Abuja anayehudumia pia nchi ya Ivory Coast, Judika Nagunwa, Kaimu Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo Ally Mayay na maafisa wengine wa wizara.