KOCHA MKuu wa Yanga, Miguel Gamondi amemtabiria makubwa mshambuliaji mpya wa timu hiyo Joseph Guede akisema atawasaidia sana kutetea mataji yote ya ndani.
Yanga ilifunga dirisha dogo la usajili juzi kwa kumtambulisha Guede raia wa Ivory Coast kama mrithi wa Hafidh Konkoni ambaye kiwango chake hakikumvutia kocha huyo raia wa Argentina.
Gamondi alisema kupata saini ya mshambuliaji huyo ni sawa na kumaliza tatizo sugu la umaliziaji ambalo limemsumbua tangu aichukue timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu.
“Naujua vizuri uwezo wa Guede, ni mshambuliaji aliyekamilika anajua kufunga lakini hata kutengeneza nafasi kwa wenzake binafsi imani yangu nikubwa kwake kitu cha msingi kwake ni kuthibitisha hilo kwa kufunga mabao yakutosha,” alisema Gamondi.
Licha ya uzoefu mkubwa aliokuwa nao kutokana na kucheza ligi mbalimbali Afrika na Ulaya,Gamondi amemtaka mchezaji huyo kupambana uwanja wa mazoezi ili kugombea nafasi ya kucheza na washambuliaji waliopo.
Alisema yeye ni kocha anayetenda haki hivyo pamoja na rekodi nzuri alizokuwa nazo kama atashindwa kujituma atamweka nje na kuwapa nafasi wachezaji wengine ambao watakuwa wanafanya vizuri mazoezini.
Guede ( 29),amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi sita akitokea timu ya Tuzlaspor FC ya Uturuki.