JULIO KUNG'ATUKA COASTAL UNION?


KOCHA Mkuu wa Coastal Union ya Tanga, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amepanga kujiunga na timu ya CDA ya Dodoma, aliyowahi kuichezea katika maisha yake ya soka kabla ya kuwa miongoni mwa nyota mahiri nchini.
Julio aliyewahi kuichezea Simba na timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, alitua Coastal Union ya Tanga mabingwa wa Bara wa mwaka 1988, mwishoni mwa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu, akichukua nafasi ya Hafidhu Badru.
Akiwa na Coastal Union, aliiwezesha kufanya vizuri katika mechi kadhaa za raundi ya kwanza na kuchanua zaidi katika raundi ya pili ambapo kwa sasa, inakamata nafasi sita kwenye msimamo wakiwa na pointi kwa pointi 35 sawa na Mtibwa Sugar, alikiwa wakiachwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Akithibitisha hilo jana kupitia kipindi cha michezo cha Radio Uhuru, Julio alisema si kitu cha ajabu kurejea katika timu yake ya zamani kuisaidia katika jitihada za kutaka kurejea Ligi Kuu.
“Sio kitu cha ajabu mimi kuifundisha CDA, timu yangu ya zamani niliyowahi kuichezea huko nyuma, nikiiacha Coastal Union katika Ligi Kuu, hiki ni kitu cha kujivunia kwa wadau wote wa Tanga,” alisema Julio.
Alisema, ingawa kwa sasa bado hajamalizana na viongozi wa timu hiyo, lakini ameamua kujiunga nayo kwa lengo la kuiwezesha kurejesha hadhi na heshima yake katika medani ya soka nchini.
Hivi karibuni, CDA ilitangazwa kuwa mabingwa wa Ligi ya Taifa Mkoa wa Dodoma, lakini wakawa wanapingwa na timu ya Maskani, wakijenga hoja kuwa wao ndio walistahili kupewa heshima hiyo.

1 Comments

Previous Post Next Post