Na Mwandishi wetu
WAKATI mkutano
mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) unatarajiwa kufanyika kesho, Katibu Mkuu wa
zamani wa shirikisho hilo, Fredrick Mwakalebela amewashauri wajumbe kujadili
masuala ya kulipatia uwezo
shirikisho hilo na kuepuka kuwa tegemezi.
Mwakalebela amesema kuwa TFF inaweza kuepukana na hali ya kuomba
fedha kwa wadau ili kusafirisha timu ya Taifa ya wanawake na baadala yake
kutengeneza sera itakayowafanya wadhamini washindani kudhamini timu na shughuli
mbali mbali bila kuingilia shughuli za mwengine.
Alifafanua kuwa
udhamini wa kampuni ya simu ya Vodacom unawazuia kampuni nyingine za
simu kama Tigo, Zantel na Airtel kudhamini timu shughuli nyingine za shirikisho
hilo na kunyimwa fursa ya kuendeleza michezo nchini.
Mwakalebela alisema kuwa TFF inatakiwa kuandaa sera ambazo
zitawaruhusu wadhamini kama hao kudhamini hata timu za taifa za vijana na
wanawake ili watanzania waweze kufaidi matunda ya uwekezaji wao.
Katibu Mkuu huyo pia alitoa ushauri kwa wajumbe hao kujadili suala la
matumizi ya uwanja wa kumbukumbu ya Karume kutumika kibiashara zaidi kutokana
na ukweli kuwa upo katika eneo zuri (Prime Area) kwa ajili ya shughuli hiyo na
kuwaingizia kipato.
Alisema kuwa eneo hilo linaweza kutumika kwa ujenzi wa
maduka, hotel na vitega uchumi mbai mbali ambavyo vitaiondolea shirikisho hilo
uhaba wa kupata fedha kwa ajili ya shughuli zake mbali mbali mbali.
Kuhusiana na kushuka kwa soka la Tanzania, Mwakalebela
aliwaomba wajumbe kujadili na kuweka mikakati mikubwa ya kuanzisha soka la
vijana wadogo kwa kushirikiana na
Cecafa, CAF na Fifa ili kufikia lengo. Alisema kuwa kwa kuandaa vijana hao,
wataweza kushindana katika mashindano ya vijana na baadaye kufanya vyema kwa
upande wa soka la wakubwa.
“Kwa sasa soka la vijana lipo jijini Dar es Salaam,
Zanzibar na pengine Arusha, mikoa
mingine ni sawa na hakuna na hii inatokana na changamoto za maeneo ya kuchezea,
hivyo mipango thabiti inatakiwa kuwekwa ili kufanikisha hilo,” alisema.
Vile vile Mwakalebela aliwataka wajumbe hao kujadili
maenedeleo ya soka la wanawake kwa kupanua wigo na kuiwezesha mikoa mengine nao
kuwa na timu za wanawake na syo kutegemea Dar es Salaam tu na hasa Kinondoni.
Alisema kuwa soka la wanawake limeonyesha kuwa ndilo
linaweza kuitoa Tanzania kimasomaso kimataifa.