Kocha Kim Poulsen anayeinoa timu ya vijana wenye umri chini
ya miaka 20 cha Tanzania (Ngorongoro Heroes) ameahidi kikosi chake kufanya
vizuri kesho kwenye mechi dhidi ya Sudan.
Akizungumza leo kwenye mkutano na
Waandishi wa Habari, Poulsen amesema timu yake imejiandaa vizuri kwa mechi hiyo
na kiu yao ni kushinda.
Kwa upande wake Kocha wa Sudan, Azhari Osman El Tahir
amesema ingawa haifahamu vizuri timu ya Tanzania, lakini wamejiandaa kushinda
kwani kwa muda mrefu walikuwa hawajashiriki mashindano ya vijana ya kimataifa.
Mechi hiyo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo
itachezwa kesho (Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa
10 kamili jioni kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh.
15,000.
Sudan iliwasili nchini jana (Aprili 19 mwaka huu) ikiwa na
kikosi cha wachezaji 20, viongozi kumi na mwandishi wa habari mmoja kwa ajili
ya mechi hiyo ya kwanza kabla ya timu hizo kurudiana jijini Khartoum kati ya
Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.
Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Brian Miiro
atakayesaidiwa na Mark Ssonko, Lee Patabali na Denis Batte wote kutoka Uganda.
Ejigu Ashenafi wa Ethiopia ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 15.
Fainali za Afrika kwa michuano hiyo zitafanyika Machi
mwakani nchini Algeria wakati za Dunia zitafanyika nchini Uturuki kuanzia Juni
hadi Julai mwakani. Katika fainali za Dunia, Afrika itawakilishwa na timu nne
za kwanza kwenye fainali za Algeria.