SINTOFAHAMU YANGA:WAZEE WAICHUKUA TIMU YAO


 Katibu wa Baraza la wazee wa Yanga, Ibrahim  Akilimali akizungumzia uamuzi wa kuichukua timu leo.

BARAZA la wazee wa klabu ya Yanga limetangaza kuichukua rasmi timu hiyo kutoka kwa uongozi uliopo madarakani chini ya mwenyekiti wake, Lloyd Nchunga. 
 Katibu wa baraza hilo Ibrahim Akilimali ameiambia mamapipiro blog  kwamba hatua hiyo inafuatia hali ya sintofahamu inayoendelea ndani ya klabu hiyo. 
Alisema kabla ya kufikia uamuzi huo walikutana na Nchunga ambaye ndiye aliwakabidhi timu hiyo hivyo waliona ni jambo la busara kwani timu ilikuwa inaelekea kubaya. 
Hata hivyo, Akilimali ambaye aliambatana na baadhi ya wazee wa klabu hiyo wakiwemo Abdallah Kibabu, Mikidadi Jagalaga, Chakupewa Bilal, Athuman Kaungu na wengineo, alisema bado Nchunga hajawakabidhi barua ya makubaliano hayo. 
“Tunashukuru kwa dhati kwa kuwa Nchunga mwenyewe alishatangaza hali mbaya ya klabu na kuthamini umoja na mshikamano na hivyo kutii kauli mbiu ya ‘Yanga Kwanza Mtu baadaye,”alisema. 
Aliongeza kuwa sintofahamu hiyo pia imepelekea timu kupoikwa ubingwa wa ligi kuu bara bila sababu, sambamba na kuwepo kwa utovu wa nidhamu uliokithiri ndani yake. 
Aidha, Akilimali alisema hata hali ya kiuchumi ndani ya klabu hiyo imekuwea mbaya kiasi cha kushindwa kusafirisha timu kikamilifu kwenye vituo na hata kuwekwa rehani meneja wa timu hiyo mjini Arusha walipokwenda kucheza na JKT Oljoro. 
“Hii ni aibu kwa kweli hadhi ya Yanga imeshuka, nidhamu hakuna na matokeo yake timu inajikuta inapata mapato kidogo inapocheza na kuacha madeni,hadi tunafikia kuweka rehani viongozi na wachezaji kuondoka Arusha kwa kutoroka,”alisema. 
Aliongeza kuwa pamoja na kuutema ubingwa watasimama kidedete kurejesha hadhi ya timu hiyo ili iweze kufanya vema katika mashindano mengine, sambamba na kusimamia zoezi la usajili wa wachezaji na mapato ya klabu. 
“Tunataka turejeshe nidhamu na hadhi ya jeshi letu kwani pamoja na ligi kuisha sisi bado niu mabingwa wa Afrika Mashariki tunahitaji kuwa na jeshi bora, pamoja na kuichukua timu pia tutasimamia mapato yote, usajili na kulipa madeni yanayoikabili klabu,”alisema. 
Aliongeza kuwa iwapo kamati ya utendaji ya Yanga ambayo ilitarajiwa kutana jana jioni itapinga uamuzi huo, watajua nini cha kufanya, ambapo kesho wanatarajia kuitisha kikao cha viongozi wa matawi yote ya Yanga kwa jili ya kuteua kamati ya mpito ya kusimamia timu hiyo. 
Hivi karibuni wajumbe wawili wa kamati ya utendajia Seif Ahmed na Sarah Ramadhan, pamoja na mjumbe wa kamati ya usajili na mashindano Abdallah Binkleb walitangaza kujitoa kwenye uongozi katika klabu hiyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa viongozi wa juu. 
Kama hiyo haitoshi, uongozi huo tangu kuchaguliwa mwezi Julai 2010 umekuwa katika msigano wenyewe kwa wenyewe ambapo mapema makamu mwenyekiti, Davis Mosha alijiuzulu kut okana nna kutoelewana na Nchunga.

Post a Comment

Previous Post Next Post