Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amepokea kwa masikitiko taarifa za shambulizi la kigaidi lililofanywa jana asubuhi (Aprili 4 mwaka huu) jijini Mogadishu, Somalia na kupoteza maisha ya Mwenyekiti wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Somalia (SFF), Said Mohamed Nur.
Kwa niaba ya TFF na wadau wa mpira wa miguu Tanzania anatuma salamu za rambirambi kwa Makamu Mwenyekiti wa SFF, Ali Said Ghuled kutokana na kifo hicho cha ghafla cha shambulizi la bomu cha Nur ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Amesema Nur alishiriki kikamilifu katika kujenga maisha ya wananchi wa Somalia kwa kupitia mpira wa miguu, hivyo analaani kwa nguvu vitendo vya kigaidi ambavyo pia vimepoteza maisha ya watu wengine katika tukio hilo.
Kwa kipindi chote cha maisha yake, Nur ameutumikia mpira wa miguu katika ngazi tofauti nchini kwake na ukanda huu wa CECAFA, hivyo kifo chake ni pigo kwa Tanzania, na daima itaendelea kukumbuka mchango wake katika mchezo wa mpira wa miguu.
Rais Tenga amesema TFF iko pamoja na familia ya Marehemu katika kuomboleza msiba huu mzito na kuwataka wawe na uvumilivu na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi makubwa kwao.
Kwa mechi zote za TFF zitakazochezwa katika kipindi cha siku 7 zijazo kutakuwa na dakika moja ya kusimama kimya kwa ajili ya kuomboleza msiba huo. Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema. Amina.