Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
linatoa pongezi kwa uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wa Simba kwa
kufanikiwa kuingia raundi ya pili (hatua ya 16 bora) ya michuano ya Kombe la
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Bila shaka juhudi,
ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali, wachezaji kujituma na kuzingatia
maelekezo kutoka kwenye benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Milovan
Cirkovic ndiyo msingi wa mafanikio ya Simba.
Tunaamini ushindi huo wa
Simba ni changamoto kubwa kwa wachezaji na viongozi kuhakikisha timu hiyo
inafanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa kwa vile ina uwezo
huo.
Licha ya Simba kufungwa 3-1
na ES Setif jana (Aprili 6 mwaka huu) mjini Setif imefanikiwa kusonga mbele
katika michuano hiyo kwa faida ya bao la ugenini. Simba ilishinda mechi ya
kwanza nyumbani mabao 2-0.
Katika hatua ya 16 bora, Simba itacheza na
mshindi wa mechi kati ya El Ahly Shandy ya Sudan na Ferroviario de Maputo ya
Msumbiji. Timu hizo zilitarajia kurudiana kesho (Aprili 8 mwaka huu) nchini
Sudan.
Simba itacheza mechi ya
kwanza Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Aprili 29 mwaka huu wakati ya
marudiano itakuwa ugenini kati ya Mei 11, 12 na 13 mwaka huu.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)