Mechi maalumu ya hisani kwa ajili ya kuchangia timu ya Taifa
ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo na wasanii wa filamu maarufu kama
Bongo Movie itachezwa Mei 4 mwaka huu.
Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi
hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni kwa
kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.
Twiga Stars kwa sasa hivi haina mdhamini na iko kambini
katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani inashiriki
michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na
Ethiopia jijini Addis Ababa. Fainali za AWC zitafanyika Novemba mwaka huu
nchini Equatorial Guinea.