ALIYEWAHI kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Frederick Mwakalebela ameshangazwa na shirikisho hilo kufumbia macho mgogoro unaoendelea ndani ya klabu ya Yanga.
Wanachama wa Yanga zaidi ya 700 juzi walifanya mkutano wao katika klabu hiyo na kufikia uamuzi wa kumtoa madarakani mwenyekiti wao Lloyd Nchunga kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake huku wakiteua kamati maalum itakayosimamia usajili wa wachezaji.
Mwakalebela ameiambia mamapipiro blog kwamba TFF kupitia Kurugenzi yake ya Utawala na wanachama ilipaswa kusimamia hali hiyo ya sintofahamu ambayo ilianza kuonekana tangu kupokwa pointi tatu wakati ligi kuu iikielekea ukingoni.
Alisema anashangaza na ukimya iliyonayo TFF juu ya kile kinachotokea Yanga kwani miaka ya nyuma walikuwa wakisimamia machafuko ya namna hiyo katika baadhi ya maeneo na kwa kiasi kikubwa walifanikiwa kuweka mambo sawa.
“Mimi nazungumza kama mdau wa soka kwani sifungamani na upande wowote…hivi ile kurugenzi ya utawala mbona ipo kimya au inaangalia sehemu ambazo kuna kura nyinmgi za wanachama(mikoa)?, mimi naona kwa hatua za jana (juzi) bado hawajachelewa wanaweza kuzima lolote baya ambalo linaweza kutokea,”alisema.
“Mbona zamani tuliwahi kuzima migogoro ya namna hiyo katika mikoa kama Manyara, Mara,Rukwa na hata wakati ule Simba ambapo Rubeya (Said) alijaribu kufanya mapinduzi, vilevile Yanga hiyohiyo katika utawala wa Madega (Iman) alitumwa kamamu wa kwanza Athuman Nyamlani kunusuru mambo,”aliongeza Mwakalebela.
Mwakalebela alisema TFF inawajibu wa kuingilia kati inapoona dalili zozote za vurugu kutoka kwa wanachama wake hivyo lakini mpaka sasa imeshindwa kutoa tamko lolote kuhusiana na mwenendo wa mambo ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo, Nchunga alisema kwamba hatambui maamuzi ya wanachama hao kwa kuwa yamefanywa kinyume na katiba ya Yanga na michezo kwa ujumla hivyo yeye bado ni mwenyekiti halali wa Yanga.
Alisema walichokifanya wanachama hao ni kujifurahisha tu kwa kwani ni mkutano wa kikatiba tu ndio una mamlaka ya kuung’oa uongozi na si vinginevyo.