SIMBA imeweka kando furaha ya
ubingwa wake wa ligi kuu soka Tanzania
bara na kuamua kuelekeza nguvu zake katika kombe la Shirikisho barani Afrika
(CAF) ambapo keshokutwa wanatarijiwa kwenda Sudan
kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Al
Ahli Shandy ya Sudan .
Wekundu hao wa Msimbazi
walikabidhiwa rasmi kombe la ubingwa jana baada ya kuwakandamiza mahasimu wao
wa jadi nchini Yanga mabao 5-0 katika mchezo wa mwisho la ligi kuu soka
Tanzania Bara uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Ofisa habari wa Simba Ezekiel
Kamwaga ameiambia mamapipiro blog kwamba wamefurahi kutwaa ubingwa huo lakini hawana budi
kuelekeza nguvu zao katika kombe la Shirikisho ambapo kikosi cha Simba
kinatarajiwa kuingia kambini leo jioni kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa
marudiano dhidi ya Wasudan hao utakaopigwa mwishoni mwa wiki hii.
Alisema kikosi chote cha timu
hiyo kitaingia katika hoteli ya Saphire iliyopo katikati ya jiji kujiandaa na
mchezo huo ambapo katika mechi ya kwanza iliyopigwa nchini wiki iliyopita Simba
ilishinda mabao 3-0.
Aliongeza kuwa taarifa zaidi
juu ya safari hiyo zitatolewa baada ya kanmati ya utendaji ya Simba ambayo
ilitarajiwa kukutana jana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya klabu
hiyo.
Aidha,Kamwaga amewapongeza
wachezaji wa timu hiyo kwa kujituma kadiri walizoweza na hatimaye kutwaa
ubingwa wa ligi hiyo ambayo ilijaa upinzani wa hali ya juu na hasa ikizingatiwa
kulikuwa na timu zaidi ya tatu zikiwania ubingwa huo.
Pamoja na pongezi hizo,
wachezaji wa timu hiyo wanatarajiwa kuizawadiwa ili kuwapa motisha kutokana na
kazi nzuri waliyoifanya.