KUTOLEWA kwa Simba kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho barani Africa (CAF) kumemponza beki wa Simba Victor Costa (pichani), imefahamika.
Simba ilitolewa kwenye michuano hiyo na Al Ahli Shendi ya Sudan jumapili iliyopita kwa mikwaju ya penalti 9-8, baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3.Simba ilikuwa ikongoza kwa mabao 3-0 iliyoyapa nyumbani, lakini Shendi waliyarudisha katika mchezo wa marudiano ndani ya dakika 90.
Kiongozi mmoja wa Simba aliliambia gazeti hili jana kwamba, wamechukizwa na beki huyo mkongwe kuwa uchochoro wa mabao hayo ya kizembe ambayo kama angefanya jitihada wasingeweza kufunga.
Alisema hatua hiyo inatokana na kiwango cha beki huyo kushuka sana na hilo limedhihirika katika michezo ya hivi karibuni ambayo amekuwa akipangwa kushindwa kucheza vema nafasi yake hiyo, hivyo kocha kulazimika kumpanga kama mchezaji wa akiba.
Kwa mantiki hiyo, kiongozi huyo alisema kuwa watalazimika kumpeleka kwa mkopo beki huiyo katika klabu ya Coastal Union ya Tanga ili akapandishe kiwango chake.
HIvi karibuni kamati ya ufundi ya Simba ilikutana kwa ajili ya kujadili mustakabali wa wachezaji wa timu hiyo ambapo walipendekeza kutemwa kwa Mganda Derrick Walullya na Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na nafasi zao zitachukuliwa na Mussa Mudde na Patrik Mbiyavanga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika hatua nyingine, uongozi wa Simba unatarajiwa kukutana hivi karibnuni kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuwa na kikosi mahiri ambacho kitashiriki vema kwenye michuano ya Kagame, Ligi Kuu msimu ujao na michuano mingine ya kimataifa ambayo timu hiyo itashiriki.