Jezi namba 30, aliyokuwa anavaa kiungo wa kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika klabu ya Simba, Patrick Mutesa
Mafisango kuanzi sasa haitakuwa ikitumika tena kwa heshima ya mchezaji huyo
aliyefariki Dunia usiku wa kuamkia jana, jijini Dar es
Salaam.
Hayo yalisemwa jana Mwenyekiti
wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alipokuwa akihutubia mamia ya wadau wa soka
waliohudhuria zoezi la kuuaga mwili wa marehemu Mafisango kwenye viwanja vya
Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa Uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kwenda kwao, DRC kwa
ajili ya mazishi kesho.
Heshima kama hiyo alipewa
kiungo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Marc Vivien Foe na klabu yake,
Manchester City ya England alipofariki Dunia Juni mwaka 2003, ambapo jezi namba
23 ilitunzwa moja kwa moja.
Aidha Rage alisema msiba huu
ni mkubwa kwa Simba kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ni muhimili mkubwa kwa timu
hiyo akiwashauri wachezaji na kuwa nao karibu ndani na nje ya
uwanja.
“Mafisango alikuwa na mchango
mkubwa kwa Simba na mara ya mwisho klabu kukumbumbwa na msiba mzito namna hii
ilikuwa ni mwaka 1978 ambapo Simba ilimpoteza mchezaji wake mahiri Hussein Tidwa
na ukweli ni kwamba wachezaji hawa tutawaenzi miaka yote na ndio sababu ya
kutotumia tena jezi namba 30 kwa kuvaliwa na mchezaji yoyote,” alisema
Rage.
Rage alisema licha ya umahiri
wa Mafisango Dimbani pia alikuwa mchezaji ambaye alitoa mchango mkubwa na hasa
wachezaji wawapo nje ya nchi kutokana na umahiri wake wa kujua lugha mbalimbali
ambapo alikuwa akiwasaidia wachezaji wenzake.
“Ni
pengo kubwa kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa akijua lugha nyingi ikiwemo
Kiswahili, Kingereza na Kifaransa na kuwasaidia wachezaji walipokuwa nje ya
nchi tutamkubuka sana Mafisango,” aliongeza.
Kutokana na machungu ya msiba
huo Rage alishindwa kumaliza kusoma risala fupi ya marehemu mara baada ya
kuishiwa nguvu na kumwaga machozi na kupelekea Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo
Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kumsaidia kusoma risala hiyo.
“Mafisango ni mchezaji ambaye
alikuwa akijituma nje na ndani ya uwanja na kabla ya kutua Simba Marehemu
aliwahi kucheza soka katika timu mbalimbali ikiwemo Tp Mazembe ya DRC, APR ya
Rwanda , Azam na Simba za Tanzania na pia alikuwa Nahodha wa timu ya Taifa ya
Rwanda ‘Amavubi’ alisema Kaburu.
Wakati wa kutoa heshima za
mwisho katika uwanja wa Sigara maelfu ya watu walijitokeza uwanjani hapo
wakiongozwa na mchungaji Tito Kihame ambaye aliongoza ibada ya kuuga mwili wa
marehemu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara na
viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi kutoka klabu mbalimbali za hapa
nchini.
Mukangara aliwataka wachezaji
wa Tanzania kujituma na kuwa na moyo kama ambao alikuwa nao Marehemu Mafisango
kwa kujituma na kuwa na jitihada za zaidi nje na ndani ya uwanja kama ambavyo
marehemu alivyokuwa akifanya.
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa
Simba na Watanzania kwa ujumla na tunamshukuru kwa kuvuka mipaka na kuona
umuhimu wa kuja na kucheza Tanzania na pia wachezaji wa Simba wasikate tamaa cha
muhimu waendeleze kile ambacho alikiacha marehemu,” alisema
Mukangara.
“Ukweli ni kwamba katika
familia ya soka hapa nchini tumepoteza mtu muhimu sana na tunamuombea kwa
Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani,” alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka
Tanzania TFF Angetile Osiah.
“Sisi Simba ni watani zetu na
tunakuwa pamoja katika shida na hivyo basi mimi kama kiongozi wa Yanga
nimeiwakilisha klabu nzima na tutaendelea kuwa bega kwa bega na watani zetu
katika kipindi hiki kigumu ila mchezaji Mafisango alikuwa ni mchezaji hodari
uwanjani hivyo basi anastaili kuigwa na wachezaji wengine,” alisema Selestine
Mwesigwa katibu Mkuu wa Yanga.
Nao
wachezaji mbalimbali kutoka timu ya Taifa Taifa Stars walijitokeza na kubeba
jeneza la mchezaji mwenzao na kuliingiza katika viwanja vya Sigara wachezaji hao
Juma Kaseja, Jonh Bocco, Mwinyi Kazimoto, Shabani Nditi, Amiry Maftah, Nurdin
Bakari, Agrey Moris na Juma Nyoso