BARAZA la wazee, pamoja na Vijana wa klabu
ya Yanga wameunga msimamo uliotolewa na aliyekuwa mfadhili wa zamani wa klabu
hiyo, Yusuf Manji kuhusiana na kurejea kwake kuidhamini timu hiyo.
Manji jana
aliibuka na kudai kuwa yupo tayari kurudi kuifadhili kwa kipindi cha mwaka mmoja
kwa masharti ikiwemo kuutaka uongozi wa Yanga ukubalike kufanywa uhakiki wa
mahesabu ya akaunti za Yanga ndani ya siku 90 na wakaguzi wa hesabu wa
kujitegemea kukagua hesabu za kipindi cha 2006 hadi 2012 kwa ajili ya fedha
zilizopokelewa na klabu.
Pia kuanzia sasa
na kuendelea akaunti za Yanga zichapishwe katika magazeti siku 15 baada ya
kumalizika kwa robo ya mwaka, upigaji wa kura ya maoni ndani ya siku 60 na
kuamua kama wanachama wa Yanga wanataka kuendesha kampuni ya Yanga au la, ifanye
mabadiliko ya katiba ndani ya siku 90 juu ya muundo wake wa uongozi kwa kukubali
mojawapo ya mfumo huu chini ya Katiba ya Yanga.
Mwenyekiti wa
Vijana wa Yanga, Bakili Makele alisema jana kwamba, masharti aliyoyatoa Manji ni
mazuri kwa sababu yatasaidia kuleta uwazi wa baadhi ya mambo ambayo yalikuwa
yamefichwa.
“Tunaunga mkono
masharti aliyoyatoa Manji ili kurejea tena kuifadhili Yanga kwani katika hali ya
kawaida mtu huwezi kutoa fedha bila kujua zinatumikaje…na ndilo hilo tumekuwa
tukilipigia kelele kila siku kwani wanachama tunataka mkutano wa kujua mambo
kama haya ili tujiridhishe,”alisema Bakili.
Bakili ambaye
aliambatana na wazee wa baraza la Yanga katika kutangaza uwepo wa mkutano wa
wanachama kesho makao makuu ya klabu hiyo, alisema kwamba hawana budi kukutana
ili kujadili mustakabali wa timu hiyo ambayo kwa sasa ipo katika hali mbaya ya
kifedha.
Alisema kutokana
na matatizo iliyonayo huenda mali za klabu zikakamatwa na mahakama na hatimaye
kupigwa mnada ili kuweza kulipa madeni hayo yanayofikia mil.106 ambapo kesi hiyo
ipo Mahakama Kuu.
Makele aliongeza kuwa, leo wanachama wa
klabu hiyo toka matawi mbalimbali wanatarajiwa kukutana katika tawi la Buguruni
kwa ajili ya kujadili ajenda mbalimbali ambazo watawasilisha katika mkutano huo
wa kesho.
Katika hatua
nyingine, Katibu wa Baraza la Wazee wa jklabu hiyo Ibrahim Akilimali,
amesisitiza viongozi wa kamati ya Utendaji ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake
Lloyd Nchunga kuondoka madarakani kama walivyowataka awali.
“Tunatoa agizo la
mwisho leo (jana) na kesho (leo) kwa Nchunga na wenzake kuachia ngazi, kinyume
na hapo watakuwa wamejiwekea sifa mbaya kwani jumapili mvua
itawaangukia,”alisema.
Akilimali
aliongeza kuwa tayari baadhi ya wanachama wa Yanga kutoka sehemu mbalimbali
ikiwemo Visiwani Zanzibar wameshawasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kushiriki katika mkutano huo wa wanachama..