WAKATI vinara wa ligi kuu bara Simba wakitarajiwa
kutua jijini leo tayari kwa mchezo wao dhidi ya mahasimu wao Yanga kesho kwenye
dimba la Taifa, mahasimu wao Yanga wameficha juu ya ujio wao.
Timu hizo zinatarajiwa kukwaana kwenye dimba la taifa
katika moja ya mchezo wa funga dimba la ligi hiyo itakayofikia tamati hiyo
kesho.
Akizungumza na gazeti hili jana,ofisa habari wa Simba
Ezekiel Kamwaga alisema kwamba kikosi cha timu hiyo kitatua leo kwa ndege
maalum kutoka Visiwani Zanzibar kilipokwenda kujiandaa na mchezo huo.
Alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na
wameapa kucheza kufa kupona kuhakikisha wanashinda mchezo huo ambao kama mambo
yakienda vema watatangaza ubingwa wa msimu wa 2011/2012.
“Kikosi chetu chote kipo fiti na vijan a watakuja
kesho (leo)kwa ndege maalum na kisha wataelekea katika hoteli moja ya kitalii
kwa ajili ya kusubiria mchezo wetu na Yanga,”alisema.
Kwa upande wa Yanga kupitia kwa msemaji wao Louis
Sendeu, kikosi cha timu hiyo kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani kipo katika hali
nzuri wakiendfelea na maandalizi ya mchezo huo, huku viongozi wakiwajenga zaidi
kisaikolojia.
Hata hivyo Sendeu alishindwa kuweka wazi ni lini timu
yao itarejea jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Bagamoyo na Dar es Salaam
hakuna umbali mkubwa hivyo timu itarejea siku yoyote.
Katika hatua nyingine, kiingilio cha chini katika
mchezo huo kinatarajiwa kuwa sh.5,000 kwa watakaokaa jukwaa la kijani bluu,
wakati kiingilio cha juu kitakuwa shilingi 40,000 kitakachohusisha mashabiki
watakaokaa jukwaa la VIP A.
Mashabiki watakaokaa VIPB watalipa sh.30,000, VIP B
shilingi 20,000 huku watakaokaa jukwaa la orange watalipa shilingi 10,000.