Ngorongoro Heroes inaikabili Sudan kesho (Jumamosi)
kwa staili ya kushambulia ili kuhakikisha inapata tiketi ya kusonga mbele katika michuano ya Afrika kwa
vijana wenye umri wa miaka 20. Mechi hiyo ya marudiano itachezwa Uwanja wa Khartoum, jijini hapa
kuanzia saa 2 kamili usiku kwa saa za AfrikaMashariki.
Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo leo (Mei 4 mwaka
huu), Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Kim Poulsen amesema kikosi chake ambacho jana usiku (Mei 3
mwaka huu) kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Omdurman kiko katika hali nzuri na kitatumia mfumo
wa 4-4-2.
"Nia yetu ni kushambulia toka mwanzo ili
kuwafanya Sudan wawe pia na kazi ya kuzuia badala ya kufikiria kushambulia tu. Nyumbani tuliwafunga mabao 3-1, hivyo
hapa watacheza kwa kushambulia tu.
Sisi tutazuia mashambulizi yao kwa kushambulia pia.
"Angalia mechi ya Manchester United na Manchester
City pale Etihad. Manchester United walikwenda pale
kujilinda zaidi kuliko kushambulia, hali iliyowafanya
wasitengeneze nafasi yoyote ya maana ya kufunga.
Staili hiyo iliwapa mwanya City ambao hatimaye
walishinda. Hivyo sisi hatuwezi kucheza kama United kwa tunataka Sudan wawe na kazi mbili, kushambulia na
kuzuia pia.
"Hiyo ndiyo njia ya kuwafanya wasifikirie
kutushambulia kwa muda wote, na tukipata bao mapema bila
shaka tutakuwa tumemaliza mechi. Wachezaji wangu
tayari nimewafahamisha hili," amesema Poulsen ambaye timu yake itafanya mazoezi ya mwisho leo usiku
(Mei 4 mwaka huu) kwenye uwanja utakaotumikakwa mechi kesho (Mei 5 mwaka huu).
Ingawa atajua hali kamili ya wachezaji wake baada ya
mazoezi ya mwisho leo usiku, lakini kocha Poulsen
amesema anatarajia kutumia kikosi kile kile
kilichoifunga Sudan katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi hicho kinaundwa na; Aishi Manula, Jamal Mroki,
Issa Rashid, Samir Ruhava, Dizana Ramadhan, Frank Damayo, Frank Sekule, Omega Seme, Thomas
Ulimwengu, Simon Msuva na Ramadhan Singano.
Wachezaji wa akiba ni Saleh Malande, Hassan Dilunga,
Ramadhan Khamis, Said Zege, Jerome Lambele,
Emily Mugeta na Atupele Green.
Mechi hiyo ambayo haitakuwa na kiingilio kwa
watazamaji itachezezwa na Aden Abdi Djamal wa Djibouti, na atasaidiwa na Wadjibouti wenzake Egueh Yacin
Hassan, Bogoreh Salime Fahan na Aden Ali Farah.
Kamishna ni Patrick Naggi kutoka Kenya.
Ngorongoro Heroes itaanza safari ya kurejea nyumbani
mara baada ya mechi hiyo. Itaondoka hapa saa 9 alfajiri kupitia Nairobi, Kenya na inatarajia kuwasili
Dar es Salaam siku ya Jumapili saa 3.20 asubuhi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Khartoum, Sudan
+249929316615
Mei 4, 2012