WAREMBO wanaotaka kushindana katika shindano dogo la kumsaka
mwakilishi wa Tanzania
katika mashindano ya Dunia (Miss World 2012) wameombwa kuendelea kuchukua fomu
za kushindana katika kinyang’anyiro hicho na kuzirudisha kabla ya Juni 4.
Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga
amesema kuwa wanatarajia kufanya mchujo
wa washiriki Juni 5 kwa ajili ya kubakiza warembo 10 kwa ajili ya kuwania
nafasi ya kushiriki katika mashindano ya Dunia yaliyopangwa kufanyika Agosti 18
kwenye ukumbi wa Dongsheng Fitness Center Stadium, mjini Ordos, Inner Mongolia , China .
Lundenga alisema kuwa
zoezi hilo
lilisimamishwa kutokana na zuio la Serikali na
wakati huo, jumla ya warembo 12 walikuwa wamekwisha chukua fomu za kushiriki.
Alisema kuwa muda wa kufanya mashindano hayo umekaribia na wanatarajia
kuitangaza tarehe mpya hivi karibuni.
Alisema kuwa amefurahishwa na kasi ya kuchukua na kurejesha
fomu, hata hivyo wanahitaji warembo wengi zaidi ili kuweza kupata wigo mpana
kwa ajili ya kumsaka mrembo atakayewania taji la Dunia ambalo kwa sasa lina
mikononi mwa mrembo kutoka Venezuela ,
Ivian Sarcos.
“Tunakaribia kufanya mashindano madogo hivi karibuni, hivyo
ni wajibu wetu kuwakumbusha warembo wanaotaka kuwania taji hilo kufanya hivyo kabla ya Juni 4 ili kuweza
kuingia katika zoezi la mchujo,” alisema Lundenga.
Alisema kuwa mpaka sasa jumla ya nchi 84 zimekwisha pata
wawakilishi wao kwa ajili ya mashindano hayo. Nchi 32 pamoja na Tanzania bado
hazija chagua wawakilishi wao katika mashindano hayo.
Fomu za kuomba
kushiriki zinapatikana katika ofisi za Miss Tanzania za jijini na mawakala wote
wa mashindano hayo katika mikoa ya Tanzania Bara.