Mshauri wa Mashujaa Musica King Dodoo kulia akizungumza na waandishi wa habari wakati wakimtambulisha meneja mpya wa bendi hiyo Martine Sospeter (kati) kushoto ni Rais wa Mashujaa musica, Chaz Baba.
ALIYEKUWA meneja wa bendi ya
African Stars ‘Twanga Pepeta’ Martin Sospeter ametangaza kujiunga bendi ya
Mashujaa Musica.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana, Martin alisema kwamba amejiunga Mashujaa Musica kwa ridhaa yake na
wala si kwa lengo la kuidhoofisha au kuiua Twanga Pepeta, bali kuendeleza
muziki wa dansi nchini.
Alisema hana ugomvi na
mkurugenzi wa Twanga Asha Baraka pamoja na kutangaza kuwa amemfukuza kazi
wakati akiwa mkoani Mtwara na bendi yake akimtuhumu kuihujumu bendi yake kitu ambacho
hakina ukweli na kimemuumiza sana kiasi
cha kumtoa machozi.
“juzi usiku nilishangazwa na
kauli ya mkurugenzi wangu wa Asha Baraka ambaye namchukulia zaidi ya dada yangu
akidai amenifukuza kazi kutokana kuhujumu bendi ikiwemo kushawishi wanamuziki
kujiunga na bendi ya Mashujaa, kauli ile
ilinisikitisha sana kutokana na ukweli kwamba nilimuheshimu sana na kufanya
naye kazi kwa miaka 13 iweje hii leo aje
anitolee maneno ya kunichafua katika vyombo vya habari,?
“Sijawahi kuhusika na mpango
wowote wa wasanii wa Twanga kuhamia Mashujaa na wala sikuwa nafahamu mpango huo
zaidi ya kusikia fununu za chinichini na mwishowe wasanii hao kutangazwa
kuhamia Mashujaa, hivyo napenda umma uelewe kwamba nimeondoka Twanga Pepeta na
nimekabidhi kila kilichochao kama kuna kitu nadaiwa mtu alete
uthibitisho,”alisema.
Alisema ameshasaini mkataba wa kazi usio na mipaka,
ambapo mbali na mkataba mnono, ameahidi kufanya kazi yake hiyo mpya kama
ilivyokuwa Twanga ambapo alidumu nayo kwa muda mrefu na kuchangia kufika hadi
hapo alipoachia, hivyo ameomba ushirikiano kwa uongozi, wanamuziki, Wadau na
hata ninyi mwaandishi wa habari.