MSINIHUSISHE NA MGOGORO YANGA-MOSHA


ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Davis Mosha ambaye alijiuzulu wadhifa huo, ametaka kutohusishwa na aina yoyote ya migogoro inayoendelea katika klabu hiyo, kwa kuwa alijiweka 
pembeni siku nyingi.
Akizunguza Dar es Salaam jana, Mosha alisema kwamba kumekuwa na tetesi kuwa yeye anahusika katika mgogoro unaoendelea hivi sasa katika klabu hiyo, kitu ambacho kimemshtua yeye pamoja na familia yake na jamaa zake wa karibu.
"Ikumbukwe kuwa mimi nilishajiondoa kwenye mambo ya mpira nilibakia Yanga kama mwanachama wa 
kawaida tu, sasa inashangaza pale ninapoingizwa katika migogoro ambayo siifahamu kwani hii inaniharibia heshima yangu na hata kwenye biashara zangu pia," alisema Mosha.
Alisema yeye hakuutuma uongozi umchezeshe beki wao Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyekuwa akitumikia kadi nyekundu, na hausiki na vipigo ambavyo timu yao ilipata na hivyo kupoteza ubingwa, hivyo ameomba 
wafuatwe wahusika na si yeye ambaye amejikita kwenye biashara zake.
Mosha alisema anaipenda Yanga lakini kamwe hawezi kujihusisha na kitu chochote ndani ya klabu hiyo, japo kuna wakati aliwahi kutoa nafasi kwa uongozi kuwa endapo watahitaji msaada wake kifedha waende kwa kuwa anapenda maendeleo ya timu hiyo.
Alisema ameshaanza kuzungumza na mwanasheria wake ili kuwachukulia hatua wale wote ambao watakuwa wanamuhusiha na migogoro ya klabu hiyo kwani kwa kiasi kikubwa wanaathiri biashara zake, hivyo sheria tachukua mkondo wake kwa wale wote watakaoendelea kumfuatafuata pasipo kuwa na ushahidi.




1 Comments

  1. YANGA BOMBA-UHURU BRANCHMay 5, 2012 at 10:15 PM

    huyu mchagga aache kutapatapa,yeye mwenyewe ndio labda anajihusisha na hicho kinachoitwa mgogoro wa yanga lakini hakuna mwenye muda wa kumuhusisha.


    mdau wa bomba,boston,usa

    ReplyDelete
Previous Post Next Post