Na Dina Ismail
GUMZO kubwa kwenye vyombo
vya habari takriban kwa wiki nzima iliyopita, ni sakata la beki Kelvin Patrick
Yondani wa Simba, kusaini mkataba wa kuichezea Yanga.
Yondani alisaini mkataba
huo Yanga Juni 7, akiridhia kukipiga Yanga kwa misimu miwili kwa dau la sh mil.
30.
Baada ya habari hizo kuchapishwa
magazetini na picha kumwonesha nyota huyo akisaini, Simba wakaibuka na kusisitiza, nyota huyo
angali wao kwa mujibu kwamba, Yanga imekiuka kanuni za usajili kumsajili
mchezaji ambaye bado walikuwa wana mkataba naye huku wakitishia kulifikisha
suala hilo Shirikisho la Soka la Kimataifa(FIFA).
Aidha Simba wakaenda
mbali wakilitaka Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), kufuatilia kwa undani juu ya sakata hilo kubaini mazingira ya
nyota huyo kutoka kambini.
Aprili mwaka huu Yondan
aliwahi kuhusishwa na mpango wa kujiunga na Yanga, lakini akasema bado alikuwa
ni mali
ya Simba.
Hata hivyo taarifa za
kiuchunguzi na matamshi ya Yondani
mwenyewe ni kwamba aliposaini Yanga alipewa fedha nusu, hivyo ingekuwa
rahisi kuwakana.
Kwa kubaini hatari hiyo, Yanga
wakafanya jitihada za kummalizia fedha zake na kumpiga picha Yondan akionekana akisani
risiti za malipo yake akiwa ana fedha zake mezani, pia kukabidhiwa jezi ya
mazoezi, tayari kuanza mazoezi baada ya kuvunjwa kambi ya timu ya soka ya
Tanzania, Taifa Stars.
Kwa Yondan kuonekana
akisaini risiti hizo, ilimfanya Mwenyekiti wake, Alhaj ismail Aden Rage,
kulaani kitendo hicho, akisema ni cha kihuni kwani hata waliomsainisha, si
viongozi wa Yanga.
Rage alimaanisha kuwa mtu
aliyehusika kumsajili Yondani, alipata kuwa kiongozi
wa Yanga kabla ya
kujiuzulu, hivyo sheria na kanuni za soka hazimpi uhalali mtu wa aina hiyo.
Rage anaongeza kuwa mkataba
wa Yondani kwa Yanga ni batili, kwani awali ulionyesha amezaliwa mwaka 1994, hivyo
ana umri wa miaka 17; kwa sheria za kazi, umri huo haruhusiwi kusaini mkataba.
Hata hivyo, Yanga waliifanyia
kazi dosari hiyo kwa kubadili, wakiandika kuwa amezaliwa mwaka 1984.
Rage anasema, mkataba wa
Yondani ni kiini macho kwani umeficha baadhi ya vipengele, huku pia ikionyesha
kuwa atalipwa fedha zake kwa awamu mbili.
Awamu ya kwanza, ni Desemba
30, 2013 na awamu ya pili itakuwa Februari 30, hivyo ni sawa na kusema,
atacheza bure Yanga.
Akifafanua zaidi juu ya
mchezaji huyo aliyezaliwa Oktoba 9, 1984, Rage anasema, mkataba wake awali
ulikuwa ufikie ukomo Mei 30, 2012, lakini Desemba 23, 2011, waliurefusha kwa
miaka miwili zaidi, hivyo kucheza Simba hadi mwaka 2014.
Kwa mantiki hiyo, mkataba
mpya wa Yondani kwa Simba, ulianza kutumika Juni mosi, 2012, lakini usiku wa
Juni 7, akasaini kuichezea Yanga.
Simba waliwasilisha
malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na tayari Rais wa Shirikisho
hilo, Leodegar Tenga, ameahidi kulifanyia uchunguzi suala hilo kujua kama
Yondan aliondoka kambi ya Taifa Stars kwa ruksa au alitoroka.
Tenga amewaahidi Simba,
ikibainika Yondan alitoroka kambini hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa
wahusika wote.
Hata hivyo baada ya Simba
kuja mbogo juu ya suala hilo, Yondan mwenyewe alikaririwa kukisisitiza ni mali
halali ya Yanga, amesaini mkataba wa miaka miwili kwa kitita cha sh mil 30 na mshahara
wa 800,000 kwa mwezi.
Kauli hiyo pia imeungwa
mkono na familia yake ambayo pamoja na kukiri ndugu yao huyo kusaini Yanga,
imeweka bayana soka ni ajira yake, hivyo hakuna ubaya wa Yondani kuangalia
hatma ya mustakabali wake.
Kwa maelezo hayo
yaliyotolewa na watu wenye akili timamu kusema kuwa hajasaini Simba, amesaini
Yanga ni wazi kuna walakini kwani awali alisema hajasaini Yanga, ameongeza
mkataba na klabu yake Simba!
Ikumbukwe, suala la
Yondan na Yanga si la jana wala juzi, mchezaji huyo kwa muda mrefu amekuwa
akihusishwa kujiunga na
klabu hiyo ya Jangwani.
Hii ilifanya Yondani
kutoaminiwa kwa asilimia 100 na Simba kwa madai kuwa alikuwa na mapenzi na
Jangwani.
Mashabiki wenyewe wa
Simba wamekuwa hawamkubali mchezaji huyo linapokuja suala la Yanga- kama
ilivyokuwa kwa kiungo na Nahodha wao wa zamani, Henry Joseph Shindika, ambaye
kwa sasa anacheza nchini Norway.
Lakini, Yondan alifanya mazungumzo
na Yanga kwa ajili ya kuhamia huko, tangu mwaka 2008 enzi hizo klabu hiyo ikiwa
chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Kondic, ingawa hawakufanikiwa.
Yanga wamekuwa wakirudi
tena na tena kwa Yondan bila mafanikio, na kwa sababu hiyo, hili si suala la
kushtukiza na iko siku beki huyo
atacheza Yanga hata kama
si msimu ujao.
Lakini, hata kama Yondan
ana mapenzi na Yanga, akibainika kusaini Yanga wakati bado ana makataba na
Simba, itamgharimu yeye kwanza na Yanga wenyewe.
Kwa upande mwingine, Yondan
anaweza akaamua kwenda Yanga licha ya kuwa na mkataba na Simba kutokana na
hukumu ambayo tayari amekwishapewa siku nyingi na mashabiki wa Simba.
Hukumu yenyewe ni kumwona
kama si mwenzao, wahenga walisema, lisemwalo lipo, kama halipo, linakuja!
Lakini, yamekwishatokea
masuala ya kuumiza kichwa kama hili la Yondani kusaini mara mbili tena wakati
huo kukiwa hakuna kanuni madhubuti, lakini yakapatiwa ufumbuzi.
Hapa namaanisha, jambo
hili la Yondan linaweza kumalizwa kwani limekuja kipindi ambacho, kanuni za
usajili zimekaa vizuri.
Sakata hili ni kama
ilivyokuwa kwa Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka Simba kwenda Yanga mwaka 2007.
Wakati huo, Yanga ilipomsajili
Chuji, Simba nayo ikasema ni wao kwa mujibu wa mkataba, lakini mwishowe, alicheza
Jangwani.
Naye Victor Costa
alisaini Yanga akitokea Simba, akavaa jezi kwenye Kombe la Mapinduzi Zanzibar,
aliporejea Dar es Salaam akaenda kwenye mazoezi ya Simba Kurasini, mwaka 2005.
Amri Saidi alisaini Yanga
mwaka 2001, lakini pamoja na kupewa fedha, akabaki Simba.
Ephraim Makoye alisaini Simba mwaka 2000, lakini akabaki
Yanga ingawa baadaye alicheza Simba.
Leo hii, kuna Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, pia Kamati ya Nidhamu ya TFF, kutoka kwao
tunatarajia watalipatia ufumbuzi hili la Yondan.
Baada ya hapo, tutakuwa
na fursa nzuri ya kufungua mjadala mpya.
Hata hivyo, jambo hili la
Yondani, ni kitendawili kigumu kinachohitaji umakini kukitegua. Ngoja tusubiri
kuona.
Maoni:dinazubeiry@gmail.com, 0788-344 566 au tembelea http//:mamapipiro.blogspot.com