Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego akisistiza jambo kuhusu haja ya kulipamba taifa na kazi za Sanaa za nyumbani kwenye kikao cha awali cha maandalilzi ya kampeni hiyo. Kulia kwake ni Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini Adrian Nyangamalle.
Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Bw.Nyangamalle akichangia kuhusu mikakati ya uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo kama ikifanikiwa italipendezesha taifa na kazi mbalimbali za mikono.
Wajumbe waliohudhuria kikao hicho wakifuatilia mchango wa
mmoja wa wajumbe kwa makini.
Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na
Shirikisho la Sanaa za ufundi nchini liko mbioni kuzindua kampeni ambayo
italenga kujenga msukumo wa kulipamba taifa na Sanaa mbalimbali nyumbani.
Akizungumza wiki hii kwenye kikao cha awali cha maandalizi
ya kampeni hiyo kilichofanyika BASATA jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa
baraza hilo Ghonche Materego alisema kuwa, lengo ni kuhakikisha maeneo ya miji,
majiji, manispaa, ofisi, mahoteli na mazingira mbalimbali yanaona umuhimu wa
kununua sanaa za nyumbani na kuzitumia kupamba.
“Hatujapamba kabisa kwa sanaa zetu, maeneo mengi ya miji,
kuta za maofisi, nyumba zetu na kadhalika ni matupu. Ni wazi kunahitajika
msukumo wa pekee katika kuhakikisha tunaipendezesha nchi yetu kila mahali na
Sanaa mbalimbali” alisisitiza Materego.
Kwa mujibu wa Materego, Tanzania ni nchi iliyojaaliwa vipaji
vingi na yenye historia ya pekee katika Sanaa za Ufundi hivyo ingetarajiwa
sanaa hizo kupamba kwa wingi miji, fukwe, maofisi, shule, majumba, mahoteli na
maeneo mbalimbali.
“Sasa kama wasanii tuingalie nchi yetu, tujiweke mbele
katika kuangalia namna ya kuipamba kwa Sanaa zetu.Tukichelewa itapambwa na
Sanaa za nje” aliongeza Materego.
Alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ikulu na Rais Jakaya
Kikwete kwa kutilia mkazo mapambo ya Sanaa za nyumbani na kutoa wito kwa ofisi
zingine za umma kuiga mkakati huo kwani ni aibu kutumia sanaa za nje kupamba.
“Mara baada ya Rais Kikwete kuingia Ikulu kulifanyika
ukarabati, maonesho ya Sanaa za ufundi yaliandaliwa ili kupata Sanaa za
kuipamba Ikulu yetu, hili ni jambo la faraja kwamba, na sisi tuna pa kuanzia”
alisema Materego.
Alitaja faida za kampeni ya kulipamba taifa na Sanaa za
nyumbani kuwa ni pamoja na kutanua soko la kazi
za wasanii, kulipendezesha taifa na kazi mbalimbali za mikono,
kuwathamini wasanii na nyingine nyingi.
Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayovuma kwa
Sanaa za Ufundi duniani kama michoro, vinyago, ususi na kadhalika lakini pamoja
na utajiri huo bado Sanaa hizi hazijapewa nguvu kubwa ndani ya mipaka.