Kikosi cha Taifa Stars ambacho jana
kilicheza na Ivory Coast hapa Abidjan na kupoteza kwa mabao 2-0 kinaendelea
kujinoa kwa mechi ijayo dhidi ya Gambia itakayochezwa Jumapili (Juni 10 mwaka
huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa programu ya
Kocha Kim Poulsen, Taifa Stars imefanya mazoezi leo asubuhi kwenye uwanja wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Ivory Coast (FIF) ambao uko pembezoni mwa jiji la
Abidjan.
Timu hiyo itafanya tena
mazoezi kesho (Juni 4 mwaka huu) asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea
nyumbani saa 1.30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo
itawasili Dar es Salaam, Juni 5 mwaka huu saa 1.40 asubuhi.
Kocha Kim ambaye amekuja na
wachezaji wote hapa ukiondoa wanne ambao ni majeruhi (Thomas Ulimwengu, Nurdin
Bakari, Haruna Moshi na Nassoro Masoud Cholo) amesema hivi sasa wameelekeza
akili yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Gambia.
“Safari ya kujenga timu ndiyo
imeanza. Mechi dhidi ya Ivory Coast imepita na ninawashukuru wachezaji kwa
kucheza kwa mujibu wa maelekezo na kujituma. Mpira ni mchezo wa makosa,
tumefanya makosa yaliyosababisha tuwape Ivory Coast mabao mepesi.
“Lakini kama nilivyosema
mechi hiyo imepita, hivi sasa tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Gambia. Hatuna
muda mwingine wa kujipanga na ndio maana niliamua kuja na wachezaji wote
Abidjan,” amesema Kim.
Mechi dhidi ya Gambia
itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Gambia ilitoka
sare ya bao 1-1 na Morocco katika mechi iliyochezwa juzi jijini
Banjul.
Hata hivyo, Taifa Stars
haitakuwa na nahodha wake msaidizi Aggrey Morris ambaye alionesha kadi nyekundu
dakika ya 65 baada ya kupata ya pili ya njano kwenye mechi dhidi ya Ivory Coast
iliyochezwa Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abidjan.