KOCHA
Msaidizi wa timu za taifa za vijana, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amepongeza
kurejeshwa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kiungo wa Yanga,
Athuman Iddi ‘Chuji’.
Kocha
Mkuu wa Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro, Mdenish Kim Poulsen, juzi
alitangaza majina ya nyota 21, akiwamo Chuji ambaye kwa mara ya mwisho aliitwa
katika kikosi hicho mwaka 2010, kikiwa chini ya Mbrazil, Marcio Maximo.
Julio alisema, kurejeshwa kundini kwa Chuji
kunatokana na jitihada zake binafsi, ambazo amekuwa akizionyesha katika timu
yake ya Yanga.
Alisema
Chuji ni mchezaji mzuri, mwenye kipaji na anayejituma uwanjani, lakini kipindi
cha katikati alighafirika na matokeo yake kupoteza mwelekeo, lakini baada ya
kuwekwa chini alizinduka.
“Ni nani
asiyekubali kiwango alichokionyesha Chuji katika siku za hivi karibuni na hata
ubingwa wa Kagame kwa Yanga na yeye alichangia pia kwa jitihada zake,” alisema.
Julio
aliongeza kuwa uwepo wa Chuji Stars utasaidia kwa kiasi kikubwa, kwani ni mchezaji
mzoefu, hivyo atakaposhirikiana na wenzake timu inaweza kupata mafanikio
makubwa.
Hali
kadhalika, Julio alipongeza uteuzi huo wa kikosi cha Stars, ambacho kitaingia
kambini Agosti 8 kwenye Hoteli ya Tansoma kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya
kimataifa ya kirafiki itakayopigwa ugenini Agosti 15.
Alisema
kocha amefanya jambo la maana, kuchanganya damu changa na wakongwe, hali
itakayoleta changamoto kubwa uwanjani.
Mbali na
Chuji, wengine ni makipa Deogratias Munishi, nahodha Juma Kaseja na Mwadini Ali.
Mabeki ni nahodha msaidizi, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani na
Shomari Kapombe, huku viungo ni Frank Domayo, Haruna Moshi, Mrisho Ngassa,
Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Chombo, Ramadhan Singano, Salum Abubakar na Shabani
Nditi.
Washambuliaji ni John Bocco, Mbwana Samata,
Said Bahanuzi, Simon Msuva na Thomas Ulimwengu.