MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa aliyepelekwa kwa mkopo katika
klabu ya Simba akitokea Azam aliyojiunga nayo msimu wa 2009/10
akitokea Yanga, jana alisaini rasmi mkataba wa kukipiga Msimbazi.
Kwa mujibu wa habari zilizotufikia , nyota huyo aliyewahi kuichezea Kagera Stars, amepewa gari.
Mbali ya gari la kutembelea, pia Ngasa mtoto wa mchezaji wa
zamani wa Pamba FC ya Mwanza, Halfan Ngasa, atakuwa analipwa mshahara wa sh
2,000,000 kwa mwezi.
Kiasi hicho cha mshahara, ni kama
alichokuwa akilipwa na klabu yake ya
Azam iliyomtoa kwa mkopo baada ya kukerwa na kitendo
chake cha kuonesha mapenzi yake kwa timu yake ya zamani ya Yanga.
Baada ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DR Congo ambapo Ngasa
alifunga bao moja kati ya 2-1, aliamua kuvaa jezi ya Yanga.
Kitendo hicho kimetafsiriwa kama
mchezaji huyo kukosa mapenzi ya dhati kwa timu yake ya Azam, hivyo kumtoa kwa mkopo.
Licha ya kuwaniwa na klabu za Simba na Yanga, nyota huyo ametua
Msimbazi baada ya kutoa dau la sh mil. 25, wakiipiku Yanga waliokuwa na ofa ya
sh mil. 20.
Mapema jana, Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alikana
habari kuwa Ngasa hakuwa ameshirikishwa kwenye mpango wa kutolewa kwa mkopo.
Alisema, Ngasa alijulishwa hilo na awali, bei yake ilikuwa dola 50,000
za Marekani, ingawa baadaye ilipungua hadi sh mil. 25.
“Tunaomba
ifahamike bayana kuwa Ngasa alipewa taarifa ya kuuzwa na aliombwa asaidie
kushawishi klabu anayoitaka ifike kwetu na ofa yake.
“Ngasa alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu
yoyote ambayo Azam ingeona imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa masilahi
yake ya kimkataba kati yake na
Azam yazingatiwe,” alisema na
kusisitiza:
“ Kwa maana hiyo, Azam
iliamua kumpeleka Ngasa kwa mkopo kwa klabu iliyofika na kuonesha nia ya
kumhitaji (Simba), ikipewa sharti la kumlipa Ngasa mshahara wake kamili (sh
2,000,000) pamoja na stahiki zake nyingine zote
za kimkataba,” alisema.
Aliongeza kuwa, kama Ngasa
anataka kuvunja mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji, watoe
dola 50,000,
kwani nyota huyo bado ni
mali ya Azam.
Kahemele alisema kama Ngasa
akiamua kubaki Azam, atakaa nje ya uwanja kwa muda wote uliosalia kwenye
mkataba, kwani hawapo tayari kumvisha jezi yao.
Mbali ya klabu ya Azam
kumwadhibu Ngasa kwa kumtoa kwa mkopo kwa kosa la kuvaa jezi ya Yanga, pia
imemtimua aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Stewart Hall.
Hall ametupiwa virago
baada ya kukaidi agizo la kutakiwa kutompanga Ngasa katika mechi ya fainali ya
Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
Katika mechi hiyo ambayo iliisha kwa Yanga kushinda mabao 2-0, Hall alimwingiza Ngasa
badala ya Kipre Tchetche.