ALIYEKUWA kiungo wa Simba Mwinyi Kazimoto jana amesaini
mkataba wa mwaka mmoja na nusu kwa ajili kuitumikia klabu ya Al Markhiya SC ya
Doha, Qatar.
Habari za uhakika kutoka Qatar zinaeleza kwamba, Kazimoto
amesaini mkataba baada ya kufaulu majaribio yake, sambamba na kukubaliana na
uongozi ofa aliyopewa.
Imeelezwa kwamba, hatua ya Kazimoto kusaini mkataba huo
imekuja baada ya uongozi wa timu hiyo kuongeza dau la kumnunua baada ya awali
kugomea kwa madai kuwa halilingani na thamani waliyomnunulia.
Chanzo hicho kimeeleza kwamba, Al Markhiya iliwaangukia
Simba kwa dau waliloafikiana kutokana na ukweli kwamba kwa sasa ipo katika hali
mbaya ya kifedha na hasa ikizingatiwa kuwa wanahitaji kusajili wachezaji
watakaoipandisdha tena daraja.
“Unajua timu imeshuka daraja hivi karibuni sasa
wanajiimarisha kwa kusajili wachezaji wazuri na fedha waliyonayo haitoshelezi
hivyo wameiomba Simba ipokee hicho walichonacho,”kilieleza chanzo hicho.
Juzi uongozi wa Simba kupitia kwa msemaji wake Ezekiel
Kamwaga ulisema umeitupilia mbali ofa iliyotumwa na klabu hiyo kwa madai kuwa
ni ya kipuuzi, huku ikidai pia Kazimoto ana maswali kwanza ya kujibu kwa
Watanzania na mashabiki wa Simba kwa ujumla.
Simba pia ilidai inakusudia kuketi na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kwa ajili ya kumjadili nyota huyo kwa kitendo chake cha kutoroka
nchini.
Kazimoto ambaye alisajiliwa na Simba mwaka juzi kutokea JKT
Ruvu, alitoroka nchini akiwa na timu timu ya Taifa iliyokuwa ikijiandaa na
mechi yake ya kufuzu fainali za Afrika zinazoshirikisha nyota wanaocheza ligi
za ndani (CHAN) dhidi ya Uganda ‘The Cranes’