TIMU ya soka ya Ruvu Shooting ya mkoani Pwani kesho inatarajiwa kujitupa katika uwanja wa wake wa nyumbani wa Mabatini kwa ajili ya
kujipima ubavu mabingwa wa soka mkoa wa Pwani, Kiluvya United.
Ofisa habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire alisema jana
kwamba mchezo huo utakaoanza saa 10 jioni ni sehemu ya maandalizi ya timu yake
kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi
Agosti 24.
Alisema mchezo huo ni muhimu sana kwao kwani kocha mkuu wa timu hiyo Charles
Boniface Mkwasa atapata kuona mapungufu yaliyoipo ili aweze kuyafanyia kazi
mapema kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.
“Kocha anatarajia kuwachezesha wachezaji wote hususani
waliosajiliwa msimu huu ili kuwa na uhakika wa uwezo na nafasi wanazozimudu
kuzicheza,”alisema
Ruvu Shooting ni miongoni mwa timu za Ligi kuu zilizosajili
vizuri kwa lengo la kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika ligi hiyo kwa kutoa
ushindano mkubwa na hatimaye kufanya vizuri katika michezo yake.
Baadhi ya wachezaji wapya iliyowaongeza ni pamoja na Cosmas Ader,
Juma Nade, Elias Maguli, Juma Seif ‘Kijiko’, Lambele Jerome, Stephano Mwasyika na
Abdul Seif Juma.