Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred
Rwiza wa Tanzania kuwa kamishna wa mechi ya raundi ya pili ya michuano ya
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Rwiza atakuwa kamishna katika mechi ya kwanza ya raundi hiyo
itakayohusisha mshindi wa mechi kati ya Msumbiji na Namibia dhidi ya Angola
itakayochezwa kati ya Agosti 9 na 11 mwaka huu. Mechi hiyo itachezeshwa na refa
Noram Matemera kutoka Zimbabwe.
Matemera atasaidiwa na Wazimbabwe wenzake Tapfumaney
Mutengwa atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba moja, Ncube Salani ambaye ni
mwamuzi msaidizi namba mbili wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni
Ruzive Ruzive.