Wanamichezo
wawili walioomba kuwania uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu wamewekewa pingamizi.
Waliopingwa
ni Wallace John Karia anayeomba kupitishwa kuwania urais na Vedastus Kalwizira
Lufano anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili ambayo
ni mikoa ya Mara na Mwanza. Anyempinga Karia ni Shamsi Rashid Kazumari wa Dar
es Salaam wakati Lufano anapingwa wa Samwel Nyalla wa Mwanza.
Pamoja na
mambo mengine, Kazumari anampinga Karia kwa madai kuwa akiwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ligi, aliwashawishi wajumbe wenzake kuingia mkataba na Azam Tv wakati
akijua kamati hiyo ni ya muda, hivyo haina nguvu za kisheria kusaini mkataba
huo.
Naye Nyalla
ambaye pia ni mmoja wa wanamichezo waliojitokeza kuwania ujumbe kupitia Kanda
hiyo anampinga Lufano kwa madai hana uzoefu wa miaka mitano katika uongozi wa
mpira wa miguu.
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu Mbezeleni itakutana kesho
(Agosti 28 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kusikiliza pingamizi hizo ambapo
wawekaji pingamizi na waliopingwa wanatakiwa kufika wenyewe ndani ya muda kwa
vile uwakilishi hautakiwi.