Usaili wa waombaji uteuzi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) unaendelea na
unatarajia kukamilika leo (Septemba 1 mwaka huu).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu
Mbwezeleni ilianza usaili juzi (Agosti 30 mwaka huu) ambapo matokeo ya usaili
yanatarajiwa kutangazwa keshokutwa (Septemba 3 mwaka huu).
Kati ya Septemba 4 na 6 mwaka huu, Kamati ya Uchaguzi
kupitia Sekretarieti ya TFF itawasilisha kwenye Kamati ya Maadili ya TFF mashauri
yote ya maadili ili kujadiliwa na kutolewa uamuzi na kamati hiyo.
Vilevile kati ya Septemba 4 na 6 mwaka huu ni kipindi cha
kukata rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kwa masuala yasiyo ya
maadili. Kwa watakaokata rufani wanatakiwa kuambatanisha na ada ya rufani kwa
Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili jioni ya Septemba 6 mwaka huu.