Na Dina
Ismail
SHIRIKISHO
la soka Tanzania (TFF) miaka kadhaa
iliyopita liliweka kanuni ya kila timu inayoshiriki ligi Kuu soka Tanzania Bara
kuwa na timu za Vijana, yaani ile ya miaka chini ya 17 na 20.
TFF ilifanya
hivyo kwa minajiri ya kuinua na kuendeleza soka la Tanzania, pia kusaidia
kupatikana kwa hazina ya wachezaji kwa ajili ya baadaye.
Kama hiyo
haitoshi, ilianzisha ligi maalum ya timu hizo za vijana ambayo imekuwa
ikifanyika kipindi ambacho mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara unakuwa umesimama.
Kwa kiasi
kikubwa michuano hiyo imekuwa ikileta na msisimko mkubwa kutokana na wachezaji
wa timu husika kuonesha vipaji vya hali ya juu.
Pia kupitia
michuano hiyo, kumetoa nafasi kwa viongozi wa timu zao kuona wachezaji ambao
wanafaa kupandishwa hadi timu za wakubwa.
Lakini,
ukiangalia ama kufuatilia kwa umakini utabaini kwamba baadhi ya timu hizo za
vijana ‘zipo zipo’ kwani hata lengo la
kuinua na kuendeleza vipaji halitiliwi maana.
Kwamba, timu
za vijana zipo lakini kipindi cha usajili viongozi wanahaha kusaka wachezaji
toka Simba, Yanga, Azam, Kagera Sugar na kadhalika badala ya kupandisha
wachezaji wa timu zao za vijana.
Ni sawa kwao
kusaka wachezaji wenye uzoefu, lakini angalau wangekuwa wanachukua hata
wachezaji watano kutoka katika kikosi cha cha vijana na kasha nafasi zingine
ndio kusaka magwiji na wale wa kigeni.
Kwani bila
ya kuwapandisha katika kikosi cha wakubwa itakuwa ni sawa na kuuwa vipaji vyako
na kuzidi kudumaza soka la Tanzania.
Kama hiyo
haitoshi, kupandisha daraja wachezaji wa timu hizo za vijana kutasaidia kubana
matumizi kwa kiasi fulani kwani tumeshuhudia mamilioni ya pesa yakitumika
kusajili wachezaji wazoefu na wale ‘mapro’.
Swali la
kujiuliza, kuna faida gani ya kuwa na timu za vijana kama hawawezi kupandishwa
madaraja, mwisho wa siku inakuwa mchawi wa soka ni timu zenyewe kwani
zinashindwa kuvuna matunda yake na kwenda kusaka ya nje.
Angalau
tunaona baadhi ya wachezaji waliopandishwa kutoka timu za vijana wakichanua katika
timu zao kwa misimu kadhaa lakini baada ya muda wanapotea katika medani ya
soka.
Baadhi ya
wachezaji kama Frank Domayo , Haruna Chanongo, Ramadhan Singano, Jonas Mkude,
Hassan Isihaka, Peter Manyika na wengineo ni baadhi ya matunda ya timu za
vijana katika Ligi Kuu Bara.
Kama hiyo
haitoshi, majina ya wachezaji hao yalikuwa chaguo la mara kwa mara katika
vikosi vya timu ya Taifa kwa nyakati tofauti.
Sijui tatizo
ni nini, kwani kwa sasa moto wa nyota hao chipukizi umezimika ghafla na wengi
wameachwa katika timu zilizowapandisha, huku wengine wakiishia kukosa namba
katika kikosi cha kwanza.
Na kwa hali
ilivyo itawawia vigumu sana kurejesha hadhi yao kama ilivyokuwa mwanzo na hiyo
inatokana na mfumo wa soka la Tanzania ulivyo.
Tulitaraji
viwango vyao vingedumu kwa muda mrefu kama ilivyokuwa enzi za kina Sekilojo
Chambua, Madaraka Suleiman, Mohammed Manyika, George Masatu, Mohammed Hussein
‘Mmachinga’ na wengineo, lakini imekuwa tofauti na sasa hivi tunaweza kusema ‘wapo wapo’.
Thomas
Ulimwengu na Mbwana Samatta ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji ‘chapuo’ la timu
za vijana, kwani hawa wana vipaji pia kama walivyo wenzao lakini wasimamizi wao
walisoma alama za nyakati, na leo hii ni ‘habari nyingine’.
Nadhani ni
wakati muafaka kwa vilabu vya ligi kuu kuiga wa nchi zilizopiga hatua katika
medani ya soka ambazo kuwapa nafasi zaidi wachezaji vijana ambao wakisimamiwa
vema wataleta manufaa katika siku za usoni.
Tunaona
wachezaji wengi nyota wa Ulaya wameibuka wakiwa wadogo na wamejitahidi kwa
kiasi kikubwa ‘kumantain’ viwango vyao kwa muda mrefu na hatimaye ili tuweze
kuwa na mafanikio katika soka.
Lakini kwa
Tanzania bado hatuwatilii maanani wachezaji chipukizi,na tumekuwa tukikumbatia
wachezaji wakongwe tu ambao baadhi yao hawana hata viwango vikubwa kama ilivyo
kwa vijana lakini tunaona wakipewa nafasi.
Kwani hata
hao waliobahatika kuwemo wameshindwa kulelewa ipasavyo matokeo yake wamejikuta
wakiishia katika pasi na kufika safari yao.
Kwa hali
hiyo nashindwa kuelewa faida ya kuanzishwa kwa timu B maana uwepo wake ni kama
kutimiza wajibu tu!