Na Dina
Ismail
GOLIKIPA mkongwe wa Tanzania, Ivo Mapunda wiki
iliyopita alifungua kituo maalum cha kuibua na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana wadogo wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi 18.
Kituo hicho
kilichopo maeneo ya Mwanagati, Kitunda huko jijini Dar es Salaam kitajulikana
kama Ivo Mapunda Sports Center.
Katika miaka
ya hivi karibuni, kumekuwa na urasimu wa
uwepo wa vituo vingi vya namna hiyo kwani vingi
‘vipovipo’ tu kwa vile wachezaji wengi wazuri ambao wanatamba na
kufanya vema katika medani ya soka nchini hawatokei huko.
Nchi zilizoendelea
katika soka zina utitiri mwingi wa vituo vya namna hiyo hivyo kuwepo kwa
ushindani wa wachezaji ambao wamepitia huko pindi wanapofanikiwa kuanza kucheza
soka la ushindani, tofauti na hapa nchini ambapo wachezaji wengi wanaibuka wakutokea
mitaani.
Kwamba
matokeo yake tumekuwa tukitegemea
wachezaji wale wale, hali inayofanya soka la Tanzania lizidi kudumaa na matokeo
yake kushindwa kufurukuta kwenye medani za
kimataifa.
Ivo Mapunda
anasema anaamini ujio wa kituo hicho utasaidia kuleta changamoto katika medani
ya soka na hasa ikizingatiwa amepata
kuwamo katika timu mbalimbali hivyo anaamini atazalisha vipaji stahili.
“Nimekuwa mchezaji ndani na nje ya nchi kwa miaka mingi
hivyo kwa uzoefu wangi nitawapa mbinu nzuri za kuwafanya waweze kufika mbali
baada ya kumaliza mafunzo yao katika
kituo change,”anasema
Mapunda ambaye alipata kuzidakia timu kongwe anasema
anaongeza kuwa kituo hicho pia “nimeanzisha kituo hiki ili kusaidia vijana
wasio na kazi hivyo itasaidia kupata ajira kupitia michezo,”anaongeza
Anasema
pamoja na mafunzo ya soka kituo hiko kitakuwa kikiwapa ushauri wa kujitambua
vijana hao ili iwe rahisi kwao kukabiliana na changamoto watakazokutana nazo
katika safari zao za kucheza soka la kiushindani.
“Ni
matumaini yangu vijana watakaotoka hapa watakuwa katika ngazi nyingine,
nimedhamiria kuleta mapinduzi katika vituo vya vijana, hivyo ninaomba sapoti ya
wazazi na Watanzania kwa ujumla ili tuweze kuzalisha wachezaji
wazuri”,anaongeza Mapunda
Ivo Philip
Mapunda ni mmoja ya makipa waliojijengea heshima hapa nchini ambaye kwa sasa
hachezi soka la ushindani tangu alipoachwa na klabu yake ya Azam mwaka 2015 na
hivyo amekuwa akifanya mazoezi mtaani kwa ajili ya kujiweka fiti.
Mapunda ambaye
aliwahi kuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, pia amepata kuzidakia pia timu
za Gor Mahia ya Kenya, St.George ya Ethiopia na Congo United kwa nyakati
tofauti.