Joseph Kaniki 'Golota'
Na Dina
Ismail
TANZANIA
imejaliwa kuwa na vipaji vya hali ya juu katika michezo na hasa mpira wa miguu
lakini imeshindwa kufanya vema katika medani za kimataifa.
Wengi wa
wachezaji ambao walibahatika kufikia hatua ya kucheza hadi timu ya Taifa wameshindwa kudumu kwa muda mrefu kama ilivyo
kwa nchi nyingine zilizoendelea licha ya kuwa na uwezo mkubwa.
Haijajulikana
sababu hasa ya wachezaji wengi wazuri
kutodumu kwa muda mrefu kucheza soka ushindani
licha ya umri wao kuwa bado unaruhusu na pia kuwa na vipaji.
Ukiangalia
kwa haraka haraka kinachopelekea hali hiyo ni utovu wa nidhamu pamoja na mfumo mzima wa uongozi wa soka hapa nchini.
Hali hiyo
imekuwa ikishika kasi katikati ya miaka ya 2000 ambapo tumeshuhudia wachezaji
wengi wazuri ambao walikuwa wakifanya vema katika timu mbalimbali na hasa za
Ligi Kuu.
Katika makala
hii tutawazungumzia baadhi ya wachezaji waliopo kwenye kundi hilo ambao kutokana na
changamoto mbalimbali huenda mpaka hii leo wangekuwa ni baadhi ya nyota
waliomo kwenye kikosi cha timu ya Taifa au kucheza soka la kulipwa.
Emmanuel Gabriel Mwakyusa:
Jina lake
lilipata umaarufu zaidi mwanzoni mwa miaka ya 2000 aliposajiliwa na Klabu ya
Simba kutoka klabu ya Nazareth ya Njombe.
Mshambuliaji
huyo mwenye nguvu na kasi ya ajabu awapo uwanjani alikuwa ni mmoja ya wachezaji
wa Simba ambao waliiwezesha kufanya vema kwenye michuano ya kitaifa na
Kimataifa.
Gabriel ambaye
alipachikwa jina la Batigol akifananishwa na nyota wa Kiargentina Gabriel Batistuta
‘Batigol’, aliitumikia klabu ya Simba kabla ya kuuzwa katika klabu ya Fanja ya
Oman.
Nyota huyo
pia amepata kuzitumikia klabu za AFC ya Arusha na Prisons ya Mbeya kwa nyakati
tofauti, tangu alipoondoka Simba nyota yake ilififia licha ya umahiri aliokuwa
nao.
Batigol
ambaye alijizolea umaarufu zaidi kutokana na kufunga mabao kwa kichwa kupitea
kwake pia kulichangiwa pia baada ya kupata majeraha kwa muda mrefu na hivyo
baada ya kupona ameshindwa kurudi katika fomu.
Amir Maftah:
Ni mmoja ya mabeki
mahiri hapa nchini ambaye alipata kuzichezea klabu kongwe hapa nchini, Simba na
Yanga kwa nyakati tofauti.
Maftah aliyesajiliwa Simba mwaka 2011 baada ya
kutemwa Yanga ni mmoja ya mabeki mahiri nchini ambaye amekuwa akitumika vema
katika klabu anazozitumikia pindi awapo uwanjani.
Beki huyo wa
kushoto ambaye pia alipata kuitumikia timu ya Taifa kwa nyakati tofauti, aliibukia
katika klabu ya Pamba ya Mwanza kwa sasa anaitumikia klabu ya Friends Rangers
ambayo inashiriki Ligi daraja la kwanza.
Licha ya
umahiri na kipaji alichonacho, Maftah ni
mmoja ya wachezaji wazuri ambao bado hajafikia hatua ya kuangukia katika ligi daraja la kwanza.
Joseph Kaniki ‘Golota’:
Mashabiki wa
soka bado wanalikumbuka sana jina lake kutokana na umahiri alikuwa nao enzi
akiicheza soka hapa nchini katika klabu ya Simba na timu ya Taifa.
Umahiri wa
mshambuliaji huyo mwenye nguvu na kasi awapo uwanjani ulimuwezesha kuipa
ushindi mnono timu yake pindi anapopangwa.
Akiwa ni
mmoja ya wachezaji waliochangia mafanikio ya Simba katika miaka ya mwanzoni mwa
2000, soka lake lilianza kushuka baada ya kuhusishwa na vitendo vya utovu wa
nidhamu.
Baada ya
kutoka Simba, alizichezea kwa nyakati tofauti klabu za Mtibwa Sugar ya
Morogoro, Al tali’aa ya Misri na Rayon ya Rwanda na klabu ya daraja la pili
KonyaSpor (KIF) nchini Sweden.
Golota
ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka saba na nunsu nchini Ethiopia
baada ya kukamatwa mwaka 2012 nchini humo akiwa na dawa za kulevya ni mmoja ya
wachezaji ambao wangeweza kuwa kwenye
timu kubwa za ligi kuu akicheza soka la ushindani mpaka sasa.
Nsa Job Mahinya:
Ni mmoja ya
wachezaji wenye vipaji vya aina yake ambaye umahiri wak ulimuwezesha kujipatia
umaarufu mkubwa nchini.
Job ambaye alipata kuzitumikia klabu kongwe za
Simba na Yanga kwa nyakati tofauti ni mmoja ya washabuliaji wanaotumia vema
uwezo wao wapatapo nafasi uwanjani.
Umahiri wake
ulimuwezesha kuitumikia pia timu ya Taifa kwa nyakati tofauti lakini jina lake
lilipotea baada ya kupata majeruhi akiwa klabu ya Azam Fc.
Pia amepata
kuzitumia klabu za Azam Fc, Moro United na African Sports ya Tanga.
Boniface Pawasa:
Mashabiki wa
soka nchini bado wanamkumbuka beki huyu kisiki wa zamani wa klabu ya Simba na
timu ya Taifa.
Pawasa
ambaye alijunga na Simba mwanzoni mwa miaka ya 2000 akitokea CDA ya Dodoma ni
mmoja ya wachezaji waliokuwa tishio uwanjani kutokana na kuwa na uwezo mkubwa
wa kuhimili vishindo vya timu pinzani .
Hata hivyo
nyota ya mchezaji huyo ilianza kupotea katikati ya miaka ya 2000 baada ya Simba
kumsimamisha kabla ya kumuacha kabisa kwa madai ya utovu wa nidhamu na kisha nyota huyo kutimkia nchini Rwanda na
Uarabuni kucheza soka la kulipwa kwa nyakati tofauti.
Pawasa
alipata kuwa mmoja ya wachezaji wa kwanza ambao waliipandisha Azam Fc kutoka
Ligi Daraja la kwanza hadi Ligi Kuu Bara.
Kwa kipaji
alichonacho angekuwa ni mmoja ya wachezaji ambao wangekuwa gumzo katika medani
ya soka mpaka sasa.
PAwasa kwa
sasa hachezi soka ya ushindani huku akijikita zaidi katika kujiendeleza katika
hatua ya ukocha wa soka.
Victor Costa:
Jina lake
halisi ni Victor Nampoka, ni moja ya mabeki wenye nguvu na uwezo mmkubwa
uwanjani.
Costa jina lake lilipata umaarufu zaidi mwanzoni
mwa mwaka 2000 akiwa na klabu ya Simba ambapo mwaka 2003 alikuwa ni mmoja ya
wachezaji wa timu hiyo waliofanikiwa kuivua ubingwa Afrika Zamalek ya Misri.
Nyota huyo
ambaye pia alikuwa ni mmoja ya wachezaji waliokuwa wakiichezea timu ya Taifa ya
Tanzania alianza kupotea kwenye mwaka 2005 baada ya kuumia kisigino akiitumikia
timu ya Taifa.
Baada ya
kujiuguza kwa muda mrefu na kupona alitimkia nchini Msumbiji na kwenda
kuitumikia klabu ya Agasabe Disongo kwa
misimu kadhaa, kabla ya kurejea tena nchini na kujiunga na Simba.
Hata hivyo,
jina la Costa limekuwa likipotea taratibu tangu alipoumia.
Costa
aambaye kwa sasa yupo Visiwani Zanzibar akiwa na timu yake ya zamani ya
Jang’ombe kama kocha mchezaji, alipata kuzicheza pia timu za Mtibwa Sugar,
Mwadui Fc na Ashanti United.
Ramadhan
Chombo ‘Redondo’:
Kwa sasa
anakipiga katika klabu ya Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Redondo ni
mmoja ya viungo mahiri ambao walipata kuwika miaka ya nyuma na umahiri wake
ulimfanya kuchaguliwa kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania.
Nyota yake
ilianza kung’ara mwaka 2000 akiwa katika kituo cha kukuza vipaji cha DSM youth
Centre kablya ya kutimkia nchini Norway mwaka 2003 alipojiunga na klabu ya
daraja la pili ya Lyngdal na kisha kerejea
nchini mwaka 2007 alipojiunga na Ashanti United.
Kutokana na
umahiri wake,Redondo ambaye pia humudu nafasi ya winga alinyakuliwa na Simba
mwaka 2008 ambako alidumu nayo hadi 2010 na kisha kerejea tena Azam Fc na
baadaye kutimkia nchini Msumbiji na kisha kurejea nchini alipojiunga na Mbeya
City.