VIONGOZI WA MICHEZO ZANZIBAR WAHIMIZWA KUJIENDELEZA

 Na Mwajuma Juma,Zanzibar

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Said Marine amesema ni muhimu kwa viongozi kuusoma mchezo unaosimamia ili kujijengea weledi zaidi. 

Aliyasema hayo alipofunga mafunzo ya wiki moja ya waalimu na waamuzi wa mchezo wa netiboli yaliyoandaliwa na Chama Cha Mpira wa Netiboli Zanzibar (CHANEZA) na kufanyika katika uwanja wa Mao Zedong mjini hapa. Alisema baraza limekuwa likihimiza viongozi wa vyama vya michezo kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watu wao ili waweze kuwa na uhakika na ufahamu wa kitu ambacho anakisimamia. 

Hivyo alisema kutoa mafunzo hayo ambayo yaliendana na kufundishwa sheria 21 za mchezo huo ambazo zimeongezeka mpya kutoka 13 ni jambo la busara litakalowafanya waalimu hao kuingia katika ligi wakiwa na uwelewa wa kutosha juu ya sheria.Mapema Katibu wa chama hicho Said Ali Mansab alisema mafunzo hayo yalilenga kiwafundisha waalimu hao juu ya uwepo wa mabadiliko ya sheria za mchezo huo ili watakapoingia kwenye ligi waweze kuzitambua . 

Alisema kuwa jumla ya washiriki awali walikuwa 30 lakini waliopatiwa vyeti ni 27 baada ya watatu kishindwa kuendelea kutokana na sababu tofauti. 

Nae Mwenyekiti wa chama hicho Nasra Juma aliwataka waalimu hao kujitahidi kutumia fursa za mafunzo zinazotolewa kila mara ili kukijengea uwelewa juu ya mambo mbali mbali yanayohusu mchezo huo. 

Alifahamisha kwamba kupata mafunzo na kujitokeza kuusoma mchezo ni njia moja nzuri ya kuuendeleza mchezo huo na jitihada zao ndio ambazo zitawafanya wafike mbali. 

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo Ashrak Bakar Juma kutoka timu ya Zimamoto alisema kupata mafunzo hayo ni chachu ya wao pamoja na wachezaji wao wanaowafundisha.

Nae Rahma Saleh Mohammed wa Zimamoto alisema baaada ya kupata mafunzo hayo wategemee mabadiliko makubwa katika michuano mbali mbali ya mchezo huo.

Hivyo alisema pamoja na kuwa sheria nane zimeongezeka na mpya kwao wao watakuwa mabalozi wazuri kwa wenzao pamoja na wachezaji wao kuwafahamisha ili waweze kuzielewa.

Post a Comment

Previous Post Next Post