CELEBRATE WITH TWANGA PEPETA MZALENDO PUB JAN.11



BENDI ya muziki wa dansi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta International’ imeandaa onyesho maalum kwa wadau wa muziki litakalofanyika Januari 11 kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub uliopo jengo la Millennium Tower, Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Onyesho hilo litakalojulikana kwa jina la ‘Celebrate with Twanga Pepeta’ litatumika pia kutambulisha video na nyimbo mpya zilizorekodiwa pamoja na mwanamuziki gwiji la Afrika, Bozi Boziana.
Mkurugenzi Mtendaji wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET), Asha Baraka amesema jijini Dar es Salaam kuwa, mbali ya nyimbo hizo mpya, pia watatambulisha video zao zilizorekodiwa kupitia kampuni inayomilikiwa na mshindi wa Big Brother Africa, Richard Dyle Bezuidenhout.
Baraka maarufu kama 'Iron Lady' alisema, waandishi wa habari, wacheza filamu, waigizaji maarufu na wanasoka watatumiwa mialiko maalumu katika onyesho hilo lililopangwa kuanza majira ya saa 2.00 usiku.
Baraka alisema, pia wameandaa chakula kwa wadau wa muziki, ambacho kitaanza kuliwa kuanzia muda huo na baada ya hapo muziki utaanza ikiwa ni mojawapo ya maadhimisho ya mkesha wa sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar.
"Ni onyesho la kuonyesha nini tumeandaa na mwanamuziki Bozi Boziana na vile vile kujumuika pamoja baada ya kumaliza mwaka 2010, bendi yetu inazidi kupata maendeleo makubwa pamoja na pigo kubwa la kifo cha muasisi wetu, Abuu Semhando Baba Diana," alisema Baraka.
Alisema kuwa, wataendelea kumkumbuka Semhando na hata katika onyesho hilo watamkumbuka kwa kuenzi heshima yake kwa bendi hiyo na muziki wa dansi Tanzania kwa ujumla.
Alisema, wameomba wadhamini mbalimbali ili kusaidia onyesho hilo ambalo kiingilio kitakuwa ni sh. 7,000.
Bozi Boziana amerekodi nyimbo mbili na bendi hiyo ambazo ni ‘Mapenzi Hayana Kiapo’ uliotungwa na Saleh Kupaza na ‘Kauli’ wa Rogert Hegga "Caterpillar".

Post a Comment

Previous Post Next Post