Maputo,
MABAO mawili ya mshambuliaji Jeremias Sitoe katika kila kipindi yameipatia Msumbiji (Mambas) ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika usiku (Aprili 23 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, jijini hapa.
Mechi hiyo maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa uwanja huo wa kisasa uliojengwa na Wachina na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji ilikuwa ya ushindani wa hali ya juu.
Rais Armando Guebuza wa Msumbiji ndiye aliyezindua uwanja huo.Sitoe alifunga mabao hayo dakika ya 19 na 51 karibu kwa staili ileile baada ya mabeki wa kati Aggrey Morris na Nadir Haroub 'Cannavaro' kujichanganya katika kucheza mipira mirefu aliyopigiwa mshambuliaji huyo mwenye kasi na pia kudhani ameotea.
"Ni matokeo mabaya, lakini mmecheza mchezo mzuri na ari yenu ilikuwa juu huku mkijituma vizuri. Bado tunatakiwa kuongeza umakini katika kuwahi mipira," alisema Kocha Jan Poulsen akiwaambia wachezaji wake mara baada ya mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka Swaziland.
Stars iliyocheza vizuri zaidi kipindi cha pili huku kwa muda mwingi ikiwa eneo la wapinzani wao, kulinganisha na kile cha kwanza ilifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Mambas.
Washambuliaji John Boko, Salum Machaku na Mwinyi Kazimoto walipata nafasi za kufunga kipindi cha kwanza lakini ama waliwahiwa na mabeki au mipira yao iliokolewa na kipa Joao Kampango.
Poulsen alikianza kipindi cha pili kwa kuwatoa Shabani Dihile, Mohamed Banka, Kazimoto na Machaku, na nafasi zao kuchukuliwa na Juma Kaseja, Ramadhan Chombo 'Redondo', Mbwana Samata na Julius Mrope.
Mabadiliko hayo yaliongeza kasi ya mchezo kwa upande wa Stars ambayo ilishuhudia nahodha wake Shadrack Nsajigwa na Cannavaro wakionywa kwa kadi za njano na mwamuzi Simanga Hhleko.
Mambas ambao watashiriki michezo ya All Africa Games itakayofanyika hapa Septemba mwaka huu walicheza kwa pasi fupi fupi na kuongeza kasi kila walipokuwa wakikaribia lango la Taifa Stars.
Poulsen aliwataka wachezaji kutumia vizuri wiki moja iliyobaki kwa ajili ya mapumziko, kwani atawaita tena kambini Mei 2 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya fainali za Kombe la mataifa ya Afrika zitakazochezwa mwakani Gabon- Equatorial Guinea dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mechi hiyo itachezwa jijini Bangui, Juni 4 mwaka huu.
Stars: Dihile/Kaseja, Nsajigwa, Amir Maftah, Morris, Cannavaro, Shabani Nditi, Banka/Redondo, Nurdin Bakari, Boko, Kazimoto/Samata na Machaku/Mrope.
Mambas: Kampango, Momed Hagi, Eugenio Bila, Eduardo Jumisse/Stelio Ernesto, Carlos Chimomole/Arlindo Cumaio, Sitoe/Danilo Manhonga, Samuel Chapanga/Francisco Muchanga, Francisco Massinga, Almiro Lobo, Celcisio Bonifacio na Zainadine Junior.
Timu inarejea leo saa 12.45 jioni kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.Authored byBoniface WamburaMedia OfficerTanzania Football Federation (TFF)finito...