MICHAUNO maalum kwa ajili ya kusaka vijana wenye vipaji vya soka wenye umri chini ya miaka 17 ‘Airtel Rising Stars’ inatarajiwa kuanza kesho katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Iringa na Morogoro.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Sunday Kayuni amesema kwamba shule 24 za sekondari toka katika mikoa hiyo zitashiriki katika michuano hiyo itakayoendeshwa kwa mtindo wa ligi.
Alisema kupitia michuano hiyo ambayo itashirikisha timu kutoka shule za sekondari, kutakuwa na makocha maalum ambao watakuwa wakifuatilia vipaji vya vijana ambapo katika hatua ya kwanza kila mkoa utatoa wachezaji 20 watakaounda timu ambayo itashiriki hatua ya robo fainali.
Timu zitakazoshiriki ni pamoja na Makongo, Twiga, Mpigi Sekondari na Goba (Kinondoni) ambazo zitatumia uwanja wa Makongo Sekondari, Azania, Kinyerezi , Msongola na Airwing (Ilala) vitatuamia uwanja wa Aiwing, Temeke, Kibugumo, Mbande na Jitegemee (Temeke) vitatumia uwanja wa Twalipo.
Nyingine ni KIhonda, Sua, Mwembesongo na Moro (Morogoro), Mwanza, Taqwa, Busweru na Nsumba (Mwanza) Tagamenda, Lugalo, Mlamke na Mawelewele (Iringa).
Naye Meneja uhusiano wa kampuni ya simu ya Airtel inayodhamini michuano hiyo Jackson Mbando alisema michuano hiyo ni mwanzo wa kampuni hiyo katika harakati zake za kuinua na kuendeleza michezo na hasa soka hapa nchini.
“Huu ni mwanzo tu wa harakati za Airtel katika kuendeleza mpira wa miguu ambao unapendwa sana, tutarajie ushindani mkubwa sana ili kuweza kupata vijana wenye vipaji stahili,”Alisema.
Kupitia michuano hiyo iliyozinduliwa mwezi uliopita na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United ya Uingereza Andy Cole, vijana sita wa Tanzania wataungana na wengine kutoka nchi tano za Afrika ambapo wataingia katika kliniki maalum itakayofanyijka hapa nchini.
Kliniki hiyo itakayoendeshwa na wataalam wa idara mbalimbali toka Manchester United ambapo baadaye watachagulia wachezaji watano bora zaidi ambao watakwenda Uingereza kuhudhuria mafunzo maalum katika kituo cha Manchester United.