KIUNGO
mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa, sasa hatajiunga
tena na Seattle Sounders ya Ligi Kuu ya Marekani, baada ya kile kilichoelezwa
nafasi yake imechukuliwa na mchezaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo (DRC.)
Rahim
Kangezi ‘Zamunda’, aliyemtafutia Ngassa nafasi ya kujaribiwa Seattle mwaka jana,
alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba Mkongo huyo ambaye naye alifanya
majaribio Seattle, alimvutia zaidi kocha wa timu hiyo, Sigi Schmid, ambaye akapendekeza achukuliwe
kwanza kabla ya Ngassa.
Hata
hivyo, Zamunda alisema Ngassa bado anafikiriwa na Seattle na ikitokea nafasi
nyingine ataitwa kwenda kutimiza ndoto zake za kucheza ‘majuu’.
Hii ni mara ya pili, Ngassa anafanya majaribio ‘majuu’ na
kuambiwa amefuzu, lakini hachukuliwi.
Awali, Aprili mwaka 2009, Ngassa alifanya majaribio katika
klabu ya West Ham United ya England na ikaelezwa amemvutia aliyekuwa kocha wa
klabu hiyo, wakati huo klabu hiyo ikiwa Ligi Kuu, Gianfranco Zola.
Lakini ilielezwa Ngassa ambaye wakati huo alipelekwa na Yussuf
Bakhresa England, alitakiwa kureja Afrika kujenga mwili, ingawa ‘ndio imetoka
hadi kesho’.
Julai mwaka jana, iliripotiwa kwamba Ngassa alifuzu
majaribio alipokuwa Marekani na soka yake ilimkosha mno Kocha Mkuu wa Sounders,
Sigi Schmid.
Mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
msimu uliopita, katika majaribio yake Seattle, alipewa nafasi ya kucheza katika
mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United ya England kwa dakika 14, siku
hiyo Sounders ikifungwa mabao 7-0.
Katika mechi hiyo, Ngassa alikaribia kufunga bao baada ya
kumzidi ujanja Rio Ferdinand, lakini kwa bahati mbaya shuti lake ‘lilipotea
njia’.
Ngassa aliyezaliwa Mei 5, mwaka 1989 mjini Mwanza, alijiunga
na Azam FC Mei 21, mwaka jana akitokea Yanga kwa dau la jumla ya Sh milioni
108.
Kwa sasa Ngassa cheche zake zimepungua katika soka ya
Tanzania kiasi kwamba hata kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen
amesema anampa nafasi ya mwisho ya kuthibitisha uwezo wake katika kikosi
kitakachoivaa Msumbiji Jumatano.