Msafara wa Yanga utakaokuwa uwanjani kwa
ajili ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek
itakayochezwa wikiendi ijayo nchini Misri unatakiwa kuwa na watu wasiozidi
40.
Kwa mujibu wa maelekezo ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) yaliyotumwa jana Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF), ni idadi hiyo tu inayotakiwa kwa vile Zamalek
inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila washabiki.
Adhabu ya Zamalek kutocheza
mechi mbili za nyumbani za michuano hiyo bila washabiki ilitolewa Aprili 20
mwaka jana na Bodi ya Nidhamu ya CAF iliyokutana jijini Johannesburg, Afrika
Kusini.
Mechi dhidi ya Yanga ndiyo
itakayokuwa ya kwanza kwa Zamalek kuanza kutumikia adhabu hiyo iliyotakana na
washabiki wake kufanya fujo kwenye mechi ya michuano hiyo mwaka jana ilipocheza
dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Hivyo kila timu (Yanga na
Zamalek) katika mechi hiyo inatakiwa kuwa na wachezaji ambao wana leseni za CAF
kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa 2012. Pia benchi la ufundi katika kila timu
linatakiwa kuwa na watu watano.
Kwa klabu zote mbili, kila
moja imeruhusiwa kuingia na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji wasiozidi kumi.
Mbali ya klabu hizo mbili, wengine waliotajwa kuruhusiwa kuingia uwanjani ni
vijana 20 watakaofanya kazi ya kuokota mipira (ball-boys).
Mechi hiyo itachezeshwa na
waamuzi kutoka Morocco ambao ni Jihed Redouane, Rouani Bouazza na Bekkali Mimoun
wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Gihed Greisha wa Misri. Kamishna wa mchezo huo
ni Ben Khadiga wa Tunisia.