Mchezaji Sifael Orgenes
Mollel (14) amechaguliwa katika mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream
ambao uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kwenda kituo cha vipaji (centre of excellence) kilichoko Dakar,
Senegal.
Mollel kutoka kituo cha
Karume alichaguliwa katika mchakato wa mwaka jana uliofanywa na mng’amua vipaji
vya soka (scout) kutoka Hispania kwa niaba ya Aspire Football Dreams yenye makao
makuu yake Doha, Qatar.
Mpango huo wa Aspire Football
Dreams kwa Tanzania una vituo 14 na mchakato wa kusaka mchezaji mmoja kila mwaka
uhusisha vituo vyote hivyo ambapo kila kimoja kinatakiwa kuwa na watoto
wasiopungua 176.
Mbali ya Karume, vituo
vingine ni Kigamboni, Kawe, Tandika, Makongo, Ukonga, Kitunda, Mbagala,
Magomeni, Morogoro, Bagamoyo mkoani Pwani na Tabata.
Mollel atakuwa kwenye kituo
hicho cha Dakar kwa muda usiopungua miaka mitatu na anatarajiwa kuondoka nchini
Machi 6 mwaka huu. Kwa mwaka wa kwanza wazazi wake watalipwa dola za Marekani
2,500, wa pili dola 2,750 na wa tatu dola 3,000.
Mpango wa Aspire Football
Dreams ambao unafadhiliwa na mtoto wa Mfalme wa Qatar una vituo viwili vya
kuendeleza watoto wenye vipaji (centre of excellence) ambayo viko Doha na
Dakar.
Lakini mpango huo unaendeshwa katika nchi 16
tofauti duniani. Nchi hizo ni Cameroon, Costa Rica, Gambia, Ghana, Guatemala,
Ivory Coast, Kenya, Mali, Nigeria, Paraguay, Rwanda, Senegal, Tanzania,
Thailand, Uganda na Vietnam.