SIKU mbili
kabla ya kucheza mechi ya marudiano na Zamalek ya Misri, mabingwa wa soka
Tanzania Bara, Yanga, wameanza kulia kufanyiwa mizengwe kabla hata ya kwenda
huko.
Msafara wa
Yanga, uliondoka jana alfajiri kwa ndege ya Shirika la Misri, kwenda Cairo,
Misri, tayari kwa mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajiwa kupigwa
kesho kwenye uwanja wa jeshi jijini humo.
Taarifa
zilizopatikana jijini Dar es Salaam juzi, zinaeleza kuwa mizengwe hiyo ilianza
kutokea wakati wa kusaka viza za kuwawezesha kuingia nchini humo ambaPo ubalozi
uliwatilia ngumu kidogo viongozi wa Yanga.
Mmoja ya
viongozi wa Yanga alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa baada ya kupeleka
maombi yao ya viza, ubalozi ulitoa kwa watu wanne tu, huku ukidai baadhi ya
masuala kukamilishwa ili kuwapatia na wengine.
“Mimi nadhani
ile ilikuwa ni mizengwe tu ya Waarabu katika kutumaliza mapema kisaikolojia,
hivi inakuwaje mtu upeleke maombi ya jumla, halafu wachache wapitishwe na
wengine wazuiwe wakati sifa ni zilezile?”
Kiongozi huyo
aliongeza kuwa jambo hilo halikuwashtua sana kwani walishajipanga kukabiliana
na hali yoyote ambayo wangekumbana kabla na baada ya kwenda Misri; kikubwa ni
kuwa wamejipanga vema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na hatimaye kusonga
mbele.
Msafara wa watu
40 wa klabu hiyo, ambao ndani yake kuna wachezaji 20 na viongozi watano,
umeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), Alex Mgongolwa.
Wachezaji
walioondoka jana ni pamoja na Shaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Athuman Idd
‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Chacha Marwa, Godfrey Taita, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Omega Seme, Davies Mwape, Pius Kisambale, Oscar Joshua,
Haruna Niyonzima, Jerry Tegete, Job Ibrahim, Stefano Mwasyika, Kenneth Assamoh
na Shamte Ally.
Pia wamo kocha
mkuu, Kostadin Papic, Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, kocha wa makipa Mfaume
Athuman, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, Katibu Mwesigwa Selestine, pamoja
na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo, Tito Ossoro, Theonest
Rutashoborwa, Seif Ahmed na Ally Mayai
Tembele.
Katika mechi ya
awali iliyopigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam,
timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, hivyo ili Yanga iweze kusonga mbele inahitaji
kushinda au sare ya mabao kuanzia mawili.