Na Charles Ndagulla, Moshi
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia
askari wake, namba G842 PC Deogratius, akituhumiwa kukutwa na misokoto minne ya
dawa za kulevya aina ya bangi ndani ya ukumbi wa Pub Albeto mjini hapa.
Askari
huyo wa kituo cha Polisi Majengo, alikamatwa Machi 25 mwaka huu, majira ya saa
mbili usiku, baada ya kufanya fujo kwa kuwashambulia walinzi wa klabu hiyo,
pamoja na mmiliki wake, Christopher Shayo maarufu kama
Mzee Chris.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana
na Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro,
Absalom Mwakyoma, imesema kuwa, askari huyo aliingia ukumbini hapo kwa lengo la
kunywa pombe na kujiburudisha na muziki.
Mwakyoma
alisema, wakati muziki ukiendelea, mlinzi wa ukumbi huo, Rajabu Hamad
alijulishwa na wateja wengine kuwa, kuna mtu anawafanyia fujo na baada ya
kuingia ukumbini, mlinzi huyo alijikuta aking'atwa mkono na askari huyo.
Mbali
na mlinzi huyo kung'atwa kwenye mkono wake wa kulia, pia askari huyo anadaiwa
kumshambulia kwa kumpiga ngumi usoni mmiliki wa klabu hiyo na ndipo Polisi
walipoitwa na kumtia mbaroni.
Kamanda
Mwakyoma alisema kuwa, baada ya askari huyo kukamatwa na kupekuliwa, alikutwa
na misokoto minne ya bangi mfukoni mwake na kwamba, kwa sasa yupo mahabusu
wakati upelelezi ukiendendea na hatua nyingine za kinidhamu.