MABINGWA wa kihistoria Ulaya, Real Madrid wamempa raha kocha
wao Jose Mourinho kwa kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa usiku wa jana.
Baada ya kushindwa
kufika Robo Fainali kwa misimu sita mfululizo kabla ya kutua kwa Mourinho,
mabingwa hao mara tisa wa michuano hiyo, wamefuzu kwa mara ya pili chini ya
kocha huyo.
Timu ya zamani ya Mourinho, Chelsea
imeungana na Madrid katika droo ya Robo
Fainali itakayopangwa kesho baada ya wao pia kushinda 4-1 na kulipa kisasi cha
kufungwa 3-1 na Napoli ya Italia katika mchezo
wa kwanza.
Kipigo cha Italia kilichangi kocha Andre Villas-Boas
kufukuzwa, lakini kocha aliyerithi
mikoba yake, Roberto Di Matteo aliyekuwa Msaidizi wake, jana ameshinda
mechi ya tatu mfululizo tangu aishike timu.
Bao la mkwaju wa penalti la Frank Lampard dakika ya 75,
liliufanya mchezo uhamie kwenye muda wa nyongeza (deakika 120), ambako
Branislav Ivanovic akapiga bao la
ushindi na kufanya Chelsea
ishinde kwa matokeo ya jumla ya 5-4.
Droo la kesho la Robo Fainali litahusisha timu kutoka nchi
saba, ambazo ni mabingwa watetezi Barcelona, AC Milan, Bayern Munich,
Marseille, Benfica na APOEL timu ngebni katika hatua hii.
“Baadhi ya timu kubwa kama Manchester United, Arsenal au
Inter Milan hazipo,” alisema Mourinho, ambaye alitwaa ndoo hiyo akiwa na FC
Porto mwaka 2004 na Inter Milan
2010.
Katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, Gonzalo Higuain
aliifungia Madrid
bao la kwanza dakika ya 26 baada ya kupokea pasi ya Kaka.
Shuti kali la mbali la Ronaldo lilidondoshewa nyavuni na
kipa Sergei Chepchugov dakika ya 55.
Karim Benzema naye alitumbukiza nyavuni dakika ya 70, kabla
ya Zoran Tosic kuwafungia wageni dakika saba baadaye.
Lakini Benzema akamsetia Ronaldo kufunga la nne dakika za
lala salama.
Akitoka kufunga bao lake la 100 katika Ligi Kuumwishoni mwa
wiki, Didier Drogba aliifungia Chelsea
bao la kwanza dakika ya 29, akiunganisha krosi ya Ramires. Terry naye akafunga
akiunganisha kona ya Frank Lampard mwanzoni tu mwa kipindi cha pili.
Na baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Ivanovic kumgonga
mkononi Andrea Dossena, Lampard akaenda kufunga kwa penalty na kufanya sare ya
jumla ya 4-4.
Ivanovic akamaliza kazi kwa bao lake la muda waq nyongeza na
kuifanhya England
iwe na timu angalau katika Robo Fainali.