Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limerejesha tena mashindano ya Kombe la FA (TFF) kuanzia msimu ujao 2012/2013
ambapo bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe
la Shirikisho.
Timu zinazotakiwa kushiriki
michuano hiyo itakayochezwa kwa mtindo wa mtoano ni zilizosajiliwa ambapo katika
maombi yao ni lazima ziambatanishe nakala ya hati ya usajili wa klabu ambayo
itatakiwa kuidhinishwa na chama cha mpira wa miguu cha wilaya.
Ada ya fomu ya maombi ya
kushiriki ni sh. 20,000 wakati ada ya mashindano ni sh. 200,000. Usajili wa
wachezaji katika Kombe la FA ni ule ule mmoja wa kalenda ya usajili ya TFF
ambapo unaanza Juni Mosi na kumalizika Septemba 10.