RAIS wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Leodger Tenga ameshangazwa na kitendo cha wazee wa klabu ya Yanga
kutoa malalamiko yao kuhusiana na adhabu walizopewa
wachezaji wa timu hiyo na kusema kuwa walipaswa kukemea vitendo vya utovu wa
nidhamu kwani msimamo walioutoa inaonyesha wanaunga mkono wachezaji wa Yanga.
“Utu uzima dawa si sumu…haiwezekani wachezaji watende vile
halafu mzee asikemee kwani kwa kufanya hivyo inaondoa kauli mbiu ya Yanga DAIMA
MBELE NYUMA MWIKO…lakini hilo
halipo kwao,”Aliongeza Tenga.
Katika hatua nyinmgine, Tenga amesema kuanzia sasa uharibifu
wowote utakaotokea kwenye uwanja wa Taifa klabu husika italazimika kulipa
gharama ya shilinmgi milioni 10 iliyoelekezwa na Serikali.
Tenga alisema Serikali ina haki ya kutoza faini hiyo
kutokana na Watanzania kushindwa kuonyesha ustaarabu wa kuuthamini uwanja huo
uliojengwa na Serikali na badala yake wamekuwa wakiuharibu kutokana na vurugu
zisizo na maana ambazo hufanywa na mashabiki wa baadhi ya vilabu.
“Ni sawa kwa Serikali kutangaza faini kwa uharibifu
utakaotokea kwenye Uwanja wa Taifa lakini pia ifike mahali viongozi wa vilabu
husika kuwaelimisha wanachama na wapenzi wao kuacha kufanya mambo yasiyo ya
kistaarabu ndani ya uwanja kwani ni vigumu kwa TFF pekee kusimamia suala la
ulinzi ama uangalizi wa uwanja,”alisema Tenga.
Aidha, Tenga aliongeza mpira ni burudani na furaha hivyo
mambo ya kihuni yanayofanywa na baadhi ya mashabiki hayaendani na lengo la
michezo na kwa mwendo huo itafikia wakati makampuni yataacha kudhamini mchezo
huo na matokeo yake kuendelea kurudisha nyuma kiwango cha mchezo huo.