Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko
na majonzi makubwa taarifa ya kifo cha Msanii wa filamu Steven Charles Kanumba
kilichotokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi ya Tarehe 07/04/2012 baada ya
kuanguka ghafla akiwa nyumbani kwake Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
BASATA inaungana na familia za wafiwa na wasanii wote nchini
kwa maombolezo ya msiba huu mkubwa na wa kihistoria. Kufiwa na msanii huyu
mahili kwenye tasnia ya filamu ni pengo kubwa kwa familia, Sekta ya sanaa na
Taifa kwa ujumla kutokana na ukweli kuwa, aliweza kuutangaza utamaduni na sanaa
yetu nje ya mipaka.
Kanumba atakumbukwa kwa moyo wake wa kujituma na kuthamini
kazi ya Sanaa toka akiwa Kundi la Maigizo la Kaole ambapo moyo wake huo
ulimfanya awe miongoni mwa wasanii walioleta mageuzi kwenye tasnia ya filamu
kwa kuifanya kuanza kupendwa na wadau wengi zaidi.
Aidha, atakumbukwa kwa juhudi zake za kuinua vipaji vichanga
katika tasnia ya filamu ambapo mara kadhaa katika kazi alizoziandaa
alishirikisha wasanii wachanga ambao BASATA inaamini watakuja kuwa hazina kubwa
kwa taifa letu.
BASATA linatoa pole kwa familia ya marehemu na Wasanii wote
katika kipindi hiki kigumu. Ni vema wasanii wote tukatumia kipindi hiki
kutathimini kwa pamoja michango yetu katika kukuza sekta ya Sanaa ikiwa ni
pamoja na kuimarisha umoja wetu lakini pia tukiyaenzi yale yote mema
yaliyofanywa na Steven Charles Kanumba.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Steven Charles Kanumba mahali
pema peponi. AMEN
Sanaa ni Kazi Kwa Pamoja Tuikuze na Kuithamini.
Ghonche Materego
KATIBU MTENDAJI, BASATA