Washiriki wa Miss Tabata 2012 wakiwa
mazoezini Da’ West Park Tabata
Na
Mwandishi Wetu
African Stars “Twanga Pepeta” na Mashauzi
Classic “Wakali wa Kujiachia” leo usiku watakonga nyoyo za wapenzi wao
watakapotumbuiza kwenye onyesho maalum la kutambulisha washiriki wa Miss Tabata
litakalofanyika katika ukumbi wa Da’ West Park, Tabata.
Mratibu wa shindano hilo Godfrey Kalinga
alisema jana kuwa onyesho hiyo maalum limeandaliwa na Bob Entertainment na Keen
Arts chini ya udhamini wa Konyagi kwa ajili ya kusherekea sikuku ya Pasaka.
Kalinga alisema washiriki wa shindano la
urembo la Dar City Centre na wale wa Ukonga pia watawasindikiza Miss Tabata
kwenye onyesho hilo la kihistoria.
Mratibu huyo alisema kuwa
washiriki kutoka vituo hivyo viwili pia watatumia fursa hiyo kujitambulisha kwa
wapenzi wa urembo.
Kalinga alisema bendi hizo mbili zitafanya
maonyesho yao kabla ya warembo kupanda jukwaani na hata baada ya utambulisho
zitaendelea kutoa burudani kali hadi majogo huku wapenzi wao wakisherekea sikuku
ya Pasaka.
“Wapenzi wa muziki na urembo kesho (leo)
watapata fursa ya kuwaona warembo hao kabla ya kushiriki kwenye shindano la Miss
Tabata ambalo limepangwa kufanyika mwishoni mwa Mei,” alisema
Kalinga.
Mratibu huyo alisema washiriki wa Miss
Tabata wanataendelea na mazoezi katika ukumbi huo baada ya onyesho ya leo
kujianda na fainali.
Warembo wanaojiandaa na Miss Tabata ni Neema
Saleh (18), Paulina Valentine (18), Khadija Nurdin (19), Phillios
Lemi (20), Noela Michael (20), Khadija Ramadhani (18), Axer Peter (20), Rahma
Hassan (19) na Mercy Mlay (21).
Wengine ni Neema Innocent (19), Ellen Sule
(22), Willihemina Mvungi (20), Queen Issa (20), Suzanne Deodatus
(19), Everline Andrew (21), Josephine Peter (20), Nadya Omary (21), Hycalica
Joseph (18) na Jamila Omary (19).
Zaidi ya warembo 10 kutoka Tabata watafuzu
kushiriki kwenye shindano la kanda ya Ilala baadaye mwaka huu.
Mrembo anayeshikilia taji la Miss Tabata
ni Faiza Ally.
Warembo wa Tabata wamekuwa wakifanya
vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania ambapo mwaka juzi Consolata Lukosi
alishinda nafasi ya tatu kabla ya kutangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Redds.
Katika shindano la mwaka juzi Julliet William pia alishinda nafasi ya tatu
katika ngazi ya taifa.