UONGOZI
wa Bongo Movie uliohusika na uratibu wa shughuli za mazishi ikiwemo michango
katika msiba wa msanii Steven Kanumba, umeingia kwenye kashfa nzito.
Kwa
mujibu wa chanzo cha uhakika kutoka ndani ya familia ya Kanumba, kamati hiyo
imedaiwa kufanya uchakachuaji wa michango hiyo inayokadiriwa kuwa mamilioni ya
fedha, achilia mbali
vitu
kadhaa, yakiwemo magunia 32 ya mchele.
Chanzo
hicho kimeidokeza Sayari kuwa, dalili za hali hiyo zilianza kujitokeza mapema
kabisa pale mwanandugu mmoja alipoenguliwa kwenye kamati hiyo, kwa kile
kinachoelezwa, kamati hiyo kufanya jukumu hilo kwa uhuru zaidi.
Dalili
nyingine, ni kitendo cha wajumbe wa Kamati hiyo kutoweka baada ya mazishi hadi
walipofika nyumbani kwa marehemu Alhamisi usiku.
Kwamba,
pamoja na mambo mengine, kwenye kikao kilichofanyika siku hiyo kati
ya wanandugu na kamati hiyo, Mama Kanumba amezuia
kuzungumzia suala la michango.
“Mama Kanumba
ametakiwa asiseme lolote kwa Waandishi wa Habari kuhusu michango… kaelezwa kama
atafanya hivyo, huenda asipate kitu kabisa,” alisema ndugu huyo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Kamati hiyo imetoa onyo
hilo kwa vile tangu kwisha kwa maziko ya Kanumba, wamekuwa wakipata usumbufu wa
simu watu kuulizia kilichokusanywa na kilichobaki.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa, baada ya kamati hiyo
kukutana na wanafamilia kwa mara ya kwanza baada ya ukimya mrefu, ilisema
michango yote ni sh mil 51.
Kati ya fedha hizo, gharama za mazishi ni shilingi mil
48 huku kukiwa na deni la sh
mil 2 za ukarabati wa barabara Leaders kutokana na
uharibifu uliofanywa na waombolezaji.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa, walipohoji fedha
zilizochangwa kupitia M-pesa kupitia namba ambayo ilitangazwa, walielezwa
ilipatikana sh 20,000 tu.
Kilisema, kiasi hicho ni kiduchu mno kwa sababu
mashabiki wa Kanumba wa Mwanza pekee, walichanga sh 300,000.
Kilidokeza kuwa, pia kulikuwa na gunia 32 za mchele
zilitotolewa na msamaria, hazijulikani zilipokwenda.
“Licha ya kutolewa gunia 32 za mchele, hazijulikani zipo
wapi…. fikiria hata mfiwa, anakosa hata gunia moja la kwenda kuanzia maisha
mapya bila mwanaye,” kilidokeza chanzo hicho.
Kilipoulizwa kwanini hawakuweka ndugu kwenye kamati
hiyo tangu mapema, kilisema alikuwemo, lakini akaenguliwakwa kwa zengwe.
Uratibu wa msiba huo ulikuwa chini ya Kamati iliyokuwa
chini ya Gabriel Mtitu na wajumbe kama Ray, Cloud, Steve Nyerere, Hapines
Magese, Mtitu William, Jacob Steven na wengineo.
Sayari ilipomtafuta Mtitu kwa njia ya simu jana,
alisema kutokana na usumbufu ambao wanaupata kwa wengi kutaka kujua juu ya
michango hiyo ya msiba, Kamati yake imeamua kukutana na waandishi wa Habari
kesho Jumanne kuweka kila kitu bayana.
“Kuna mengi yanasema hadharani na chini ya zuria
kuhusu rambirambi, kwa lengo la kuweka bayana kila kitu, tumepanga kukutana na
waandishi wa Habari Jumanne (kesho) kuanzia majira ya saa nne,” alisema Mtitu.
CHANZO:GAZETI LA SAYARI