MECHI ya Ligi ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba na Moro
United iliyokuwa ichezwe Aprili 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam imerudishwa nyuma hadi Jumatatu ya Aprili 23 mwaka huu kwenye uwanja huo
huo na itaanza saa 1 kamili usiku.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace
Wambura amesema kwamba mabadiliko hayo yamefanyika ili kuipa Simba fursa ya
kujiandaa vizuri kwa mechi yao ya Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya Al
Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Aprili 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Alisema pia mechi kati ya Azam na Mtibwa Sugar iliyokuwa
ichezwe Aprili 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam imesogezwa
mbele hadi Aprili 22 mwaka huu kupisha mechi ya U20 kati ya Tanzania na Sudan
itakayochezwa Aprili 21 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine mbili zimefanyiwa marekebisho; Coastal Union
na Kagera Sugar zilizokuwa zicheze jijini Tanga, Aprili 29 mwaka huu, mechi yao
imesogezwa hadi Aprili 30 mwaka huu ili kupisha shughuli za Mei Mosi kwenye
Uwanja wa Mkwakwani. Nazo Azam na Toto Africans zilizokuwa zicheze Aprili 26
mwaka huu Uwanja wa Chamazi, sasa zitacheza Aprili 28 mwaka huu.